1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Upinzani Uturuki waungana dhidi ya Erdogan

7 Machi 2023

Muungano wa vyama sita nchini Uturuki uitwao Muungano wa Kitaifa, umemteua kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo kama mgombea atakayepambana na Rais Recep Tayyip Erdogan katika uchaguzi wa mwezi Mei.

Türkei Ankara Oppositionsbündnis | Kemal Kilicdaroglu CHP
Picha: ADEM ALTAN/AFP

Hatua hii imefikisha mwisho miezi ya ati ati na mivutano iliyokuwa imewavunja moyo wafuasi wa upinzani.

Makubaliano ya dakika za mwisho yaliyokuwa na lengo la kupeusha kugawika kwa kura za upinzani yameshuhudia mkuu wa chama cha Republican's People's Party CHP Kemal Kilicdaroglu, kuwateua mameya maarufu wa Istanbul na Ankara kama makamu wake wa rais iwapo lakini ataufikisha mwisho utawala wa Erdogan wa miongo miwili.

Mwafaka huo umefikiwa saa chache baada ya mwanachama muhimu wa muungano huo Meral Aksener, ambaye anakiongoza chama cha kizalendo cha Iyi na ambaye alikuwa anaupinga uteuzi wa Kilicdaroglu, kukubali suluhisho lililowekwa mezani na kurudi katika muungano huo.

Kurudi kwa mfumo wa utawala wa bunge

Aksener alikuwa amejiondoa kutoka kwenye muungano huo Ijumaa iliyopita katika hatua ambayo ingemnufaisha Erdogan pakubwa.

Kiongozi wa chama cha IYI Meral AksenerPicha: ADEM ALTAN/AFP

Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wafuasi wa upinzani, Kilicdaroglu mwenye umri wa miaka 74, amesema hawangekuwa na nafasi iwapo, kama upinzani hawangepata mwafaka na wakaishia kutengana.

"Meza yetu ni meza ya amani na udugu. Lengo letu kubwa ni kuipeleka Uturuki njia ya mafanikio, amani na siku za furaha," alisema Kilicdaroglu.

Muungano huo umeahidi kurudisha mfumo wa utawala wa bunge nchini Uturuki na kuuondoa mfumo wa urais aliouanzisha Erdogan.

Soma zaidi:Uwezo wa muungano huo wa upinzani kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu nchini Uturuki, Ankara na Istanbul, umeiondoa dhana iliyojengeka kwamba Erdogan hawezi kushindwa.

Rais huyo wa Uturuki anakabiliwa na wakati mgumu wa kupigania maisha yake ya kisiasa katika kile ambacho wengi wanakiona kama ni uchaguzi muhimu zaidi nchini Uturuki tangu taifa hilo liwe jamhuri miaka 100 iliyopita.

Kinyang'anyiro ni kikali katika uchaguzi wa Mei

Erdogan mwenye umri wa miaka 68, atahitajika kuviruka vihunzi viwili, mgogoro wa kiuchumi na matokeo ya tetemeko baya la ardhi lililoikumba nchi hiyo, wakati ambayo anatazamia kuendeleza utawala wake hadi mwaka 2028.

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: Mehmet Kaman/AA/picture alliance

Kura za maoni zinaonesha kwamba kutakuwa na ushindani mkali na bado haijulikani ni nani atakayekuwa mshindi wa wazi.

Kilicdaroglu hajashinda uchaguzi wa kitaifa katika miaka 13 ambayo amekiongoza chama cha CHP. Mameya wawili wa Istanbul na Ankara ambao wote wako katika chama chake, kupitia kura za maoni, wamekuwa wakifanya vyema katika kukabiliana na Erdogan kuliko Kilicdaroglu.

Soma zaidiKilicdaroglu alipata umaarufu baada ya kufichua madaiya ufisadi yaliyowahusisha wanachama wa chama cha Erdogan na alichaguliwa kuichukua nafasi ya mwenyekiti wa zamani wa chama cha CHP aliyejiuzulu kufuatia sakata ya ngono iliyokuwa inamkabili.

Mbali na chama cha CHP na Iyi, vyama vyengine vilivyo katika muungano huo wa upinzani ni chama cha kihafidhina cha Felicity, Democratic Party, The Democracy and Progress Party na Future Party.

Mara ya mwisho upinzani kuungana nchini Uturuki katika juhudi za kumuondoa madarakani Erdogan, ilikuwa ni katika kura za manispaa za mwaka 2019.

Vyanzo: AP/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW