Upinzani Venezuela utashiriki uchaguzi wa mikoa
1 Septemba 2021Vyama hivyo vya upinzani vimetoa tangazo hilo siku chache kabla ya upande wa upinzani na serikali kukutana Mexico kwa lengo la kuendeleza mazungumzo ya kutafuta njia ya kumaliza mkwamo wa kisiasa uliotawala Venezuela.
Pande zote mbili zilikubaliana kujadili masuala ya uchaguzi kama sehemu ya mazungumzo, yaliyoanza rasmi mapema mwezi huu.
Soma zaidi: Guaido aliomba jeshi kususia uchaguzi Venezuela
Juan Guaido, kiongozi wa muungano huo wa vyama vya upinzani wa United Platform alliance amesema wamefanya uamuzi huo baada ya majadiliano ya kina yaliyoshirikisha viongozi wa mikoa na kitaifa.
Siku chache zijazo, serikali ya Venezuela na upinzani wanapanga kuanza mazungumzo yao huko Mexico wakisaka suluhisho la mzozo wa kisasa ulioikwamisha nchi yao. Mazungumzo yalizinduliwa katika Jiji la Mexico mwezi uliopita.
Upinzani unadai kufanyike uchaguzi ulio huru pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa. Huku serikali ya kisoshalisti ya Rais Nicolas Maduro ikitaka kulegezewa vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa.
Upinzani ulisusia uchaguzi 2018
Upinzani haukushiriki uchaguzi wa mwaka 2018 kwa madai kwamba haukuwa huru na wa haki. Rais Maduro anayeiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma alishinda kwenye uchaguzi huo. Bunge lilikataa kumtambua kama rais halali wa nchi hiyo, kwa madai kwamba kulifanyika wizi wa kura wakati wa uchaguzi, vitisho pamoja na watu wachache kujitokeza katika vituo vya kupigia kura.
Kufuatia hali hiyo, Guaido, ambaye ni spika wa bunge la Venezuela alijitangaza kama rais wa mpito. Na tangu wakati huo, pande hizo mbili zimekuwa zikivutana kisiasa huku Maduro akigoma kuachia madaraka.
Soma zaidi:Maduro asema Venezuela haitasalimu kutokana na vitisho
Licha ya kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta duniani, uzalishaji wa mafuta umepungua na kufika katika viwango vya chini kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miaka 80 nchini humo.
Na hivyo raia wa Venezuela wanakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi huku watu wapatao milioni 5.6 wakiwa wameshaikimbia nchi hiyo.
Mamilioni ya watu wa Venezuela wanaishi katika umaskini kutokana na mishahara midogo na bei za juu za chakula zinazotokana na mfumuko wa bei mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.
Shirika la msaada wa chakula la Umoja wa Mataifa limekadiria kwamba mtu mmoja kati ya kila raia watatu wa Venezuela anashindwa kupata chakula cha kutosha cha kila siku.
Uchaguzi wa mikoa na manispaa umepangwa kufanyika Novemba 21.
Vyanzo: ap, dpa