Upinzani wa Syria kuamua kuhusu mazungumzo ya Geneva
27 Januari 2016Akizungumza na shirika la habari la AFP baada ya kuwasili katika hoteli ya fakhari ya mjini Ryadh, mkutano huo unakofanyika, msemaji wa "kamati kuu ya majadiliano"-HNC, Monzer Makhous, amesema mazungumzo yao huenda yakadumu siku nzima.
Wajumbe wa kamati hiyo inayoungwa mkono na Saudi Arabia wameanza kujadiliana tangu jana wakitilia mkazo wao peke yao ndio wanaobidi kuwakilisha upande wa upinzani.
Lakini wawakilishi wa makundi kadhaa mengine ya upinzani ambayo hawawakilishwi katika kamati hiyo,wameliambia shirika la habari la AFP, kwamba wamealikwa pia na Umoja wa Mataifa kushiriki katika mazungumzo Ijumaa ijayo mjini Geneva.
"Jibu litakuwa kupata ufafanuzi na sio kukubali au kukataa," amesema msemaji wa kamati kuu ya majadiliano, Monzer Makhous na kuongeza, "wanataka kujua nani wengine wamealikwa na kwa misingi gani na kipi kitakachojadiliwa."
Masuala ya kiutu ni muhimu kuliko mazungumzo ya kisiasa
Mwanachama mwengine wa kamati hiyo, Salem al Meslat anachambua: "Tunajiandaa vizuri kushiriki katika mazungumzo ya Geneva. Lakini kuna mengi bado, azimio la Umoja wa mataifa nambari 2254, vifungu nambari 12 na 23, kuna masuala ya kiutu, hayo kwetu sisi ni muhimu zaidi kuliko mjadala wowote wa kisiasa."
Ofisi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura imesema imetuma mialiko kwa ajili ya mazungumzo ya Ijumaa ijayo, lakini haikufafanua nani wataiwakilisha serikali ya rais Bashar al Assad wala upande wa upinzani nchini Syria.
Wakurd wa PYD hawatoalikwa mazungumzoni
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema hivi punde amearifiwa na de Mistura kwamba Wakurdi wa chama cha Umoja wa kidemokrasi - PYD hawatoalikwa kuhudhuria mazungumzo ya Geneva.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa ameongeza kusema amezungumza na msimamizi wa upande wa upinzani Riad Hijab aliyemhakikishia kwamba watashiriki katika mazungumzo hayo - ingawa wanahitaji ufafanuzi kuhusu wale watakaoshiriki na kile kilichotekelezwa upande wa kiutu na pia kuhusu kile kitakachojadiliwa.
Kundi jengine la upinzani - Muungano wa Taifa la Syria linashurutisha kushiriki katika mazungumzo ya Geneva na kuacha kuzingirwa maeneo pamoja na kutekelezwa masharti mengineyo nchini humo. Kundi hilo linasema linasubiri jibu la katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu madai yao kabla ya kutamka kama watashiriki au la mazungumzoni.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo