1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani waandamwa Angola

4 Aprili 2022

Dalili zinaonesha kuwa kwenye uchaguzi wa Agosti 2022, chama tawala nchini Angola, MPLA, kinaweza kuangushwa na muungano wa upinzani, lakini serikali imeanza kutumia vyombo vya dola kuzuia kushindwa.

Afrika Angola Präsident Joao Lourenco
Picha: Adrian Dennis/AFP/AP/picture alliance

"Maafisa wa polisi walikuja hapa alfajiri, wakaingia majumbani kwa nguvu bila hodi, wakafanya msako mkali dhidi ya wanasiasa wa upinzani na familia zao. Zaidi wanawasaka watu wanaohusiana na chama cha UNITA," anasema Kinkani Ngangu, mwanasiasa kutoka jimbo la Uige la kaskazini mwa Angola.

Huko wanasiasa wengi wa upinzani kama yeye wameshaonja jela, akiwemo mama mmoja kijana ambaye kama alivyo Ngangu ni mwanachama wa UNITA, ambaye anasema wanalazimika kumpelekea mtoto wake wa miezi minane kunyonyeshwa jela na kisha kurudi naye kila siku. 

Vyombo vya usalama vimekuwa vikizivamia nyumba kwenye maeneo mengi mbalimbali ya nchi, ambako misako na kamatakamata yamekuwa mambo ya kawaida sasa, miezi mitano kabla ya uchaguzi mkuu, lakini ni jimbo la Uige linaloandamwa zaidi.

Matokeo yake, wanasiasa wa upinzani wanalazimika ama kwenda mafichoni ama kukimbia kabisa. 

Maandamano ya madaktari jijini Luanda kupinga hali duni ya maisha.Picha: Privat

Felix Simao, katibu wa UNITA kwenye jimbo hilo, anasema "polisi inatumia visingizio visivyo maana" kwa kuwahusisha wanachama wa chama chake na ghasia na vurugu ambazo hazipo, ili kupata sababu ya kuwaandama.

"Tumekuwa tukiandamwa kwa kutembea tu mitaani kwa amani kuonesha mshikamano wetu na UNITA. Ni makossa kusema kwamba tunataka kusababisha matatizo. Tungelitaka fujo, tusingewachukuwa wake na watoto wetu."

MPLA inauogopa muungano wa wapinzani

Waandishi wa habari walio eneo hilo wanathibitisha madai haya ya wapinzani. Polisi huwaandama wanachama wa kawaida na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani, UNITA, wa chama cha Democratic Bloc, BD, na wa kundi lijiitalo PRA-JA, ambalo halina sifa ya kuwa chama cha siasa. 

Vikosi vya usalama vikiwakamata vijana wanaoandamana mitaani.Picha: Paulo Novais/dpa/picture alliance

Mnamo mwezi Oktoba 2021, makundi haya matatu yaliunda muungano kwa jina la FPU, ambao wafuatiliaji wa mambo wanasema una nafasi kubwa ya kukiondowa chama tawala cha MPLA, kilichoanza kama vuguvugu linalofuata mrengo wa Kimarx, na ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1975 wakati Angola ilipopata uhuru wake.

Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, kumeshafanyika chaguzi nne ambapo daima ushindi wa MPLA umekuwa mkubwa na wa wazi. Uchaguzi wa mwisho kabisa, mwaka 2017, rais wa sasa, Joao Lourenco, alitangazwa kushinda kwa asilimia 64. 

Lakini mwaka huu, mambo yanaweza kuwa tafauti, kwani watu wanaonekana kukerwa sana na serikali iliyopo na upinzani unaonekana kupata umashuhuri zaidi na umeungana zaidi. Hilo litawezekana tu ikiwa hakutakuwa na udanganyifu kwenye kura.

Kinachoendelea sasa kinaonesha utakuwapo.