1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wagawanyika Syria

13 Machi 2013

Huku makundi yanayotaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad wa Syria yakizidi kupata nguvu kwa kuteka maeneo kadhaa nchini humo na Uingereza ikisema huenda ikawapa silaha waasi hao.

Smoke rises from one of the buildings in the city of Homs March 11, 2013. Picture taken March 11, 2013. REUTERS/Yazan Homsy (SYRIA - Tags: CONFLICT POLITICS CIVIL UNREST)
Vita vikiendelea katika mji wa HomsPicha: Reuters

Marekani inasema upinzani wa Syria unaendelea kugawanyika na pia unakabiliwa na hali ya kujipenyeza kwa makundi ya wapiganaji kutoka nchi za nje.

Miaka miwili baada ya vuguvugu la kuuondoa utawala wa Rais Assad, mashirika ya ujasusi nchini Marekani hayafahamu hadi lini kiongozi huyo wa Syria ataendelea kuwapo madarakani, mkurugenzi wa ujasusi wa Marekani, James Clapper, ameiambia kamati ya baraza la seneti inayohusika na masuala ya ujasusi kuhusiana na kitisho cha usalama duniani.

Mkurugenzi wa Usalama wa taifa Marekani James ClapperPicha: Reuters

"Swali tunalojiuliza ni: 'ni kwa muda gani Assad atang'ang'ania madarakani?', na jibu letu la kawaida ni kwamba 'muda wake unakaribia mwisho.' Ni kwamba hatufahamu idadi ya siku zilizobaki. Tathmini yetu ni kwamba amedhamiria kubaki madarakani na kuendelea kudhibiti utawala wa nchi hiyo", Clapper aliliambia jopo la kamati hiyo ya seneti hapo jana.

Wapiganaji wagawanyika

Serikali ya Assad inapoteza maeneo iliyokuwa ikiyashikilia na inakabiliwa na upungufu wa watu na vifaa, Clapper amesema. Lakini wakati huo huo, kuna makundi zaidi ya mia moja ya wapiganaji wa upinzani ambao viongozi wanasumbuka kuweka uongozi wa pamoja na udhibiti.

Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: picture alliance / AP Photo

Clapper amedokeza kuwa kuna ongezeko kubwa miongoni mwa wapinzani wa Assad la wapiganaji kutoka nje, wengi wao wakihusishwa na kundi la Nusra, tawi la al-Qaida kutoka Iraq ambalo limepata nguvu nchini Syria kwa kiasi fulani kutokana na kutoa huduma kwa umma baada ya kuathirika na miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Marekani na maafisa wa Ulaya wamesema hivi karibuni kuwa serikali zao zitaongeza juhudi za kutoa msaada ambao sio silaha pamoja na mafunzo kwa makundi ambayo hayahusiani na makundi ya waasi wa Kiislamu, yanayopigana na utawala wa Assad.

Wakati huo huo Uingereza huenda ikafikiria kuipigia kura ya veto hatua ya kurefusha vikwazo vya silaha vya umoja wa Ulaya dhidi ya Syria iwapo hali haitatengemaa nchini humo, amesema waziri mkuu David Cameron jana.(12.03.2013)

Waziri mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Getty Images

Vikwazo vya umoja wa Ulaya

Umoja wa Ulaya umeweka vikwazo vya silaha kwa jumla dhidi ya kupeleka silaha nchini Syria , licha ya kuwa mwezi uliopita Uingereza iliushawishi umoja wa Ulaya kulegeza vikwazo hivyo na kuruhusu mataifa wanachama kutoa msaada ambao sio silaha kamili , kama vile magari yanayoweza kubeba silaha , kwa waasi wanaopambana na utawala wa rais Bashar al-Assad.

Uingereza na Ufaransa zimeashiria kuunga kwao mkono kuondoa vikwazo ili kuruhusu silaha kuingia nchini Syria. Muda wa mwisho wa vikwazo vya sasa vya silaha vya umoja wa Ulaya, unamalizika Mei mwaka huu.

Mwandishi: Sekione Kitojo/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW