1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani waitisha mgomo wa taifa nchini Belarus

Saleh Mwanamilongo
26 Oktoba 2020

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Belarus ametangaza mgomo wa nchi nzima ,kuongeza shinikizo kumtaka Rais Alexander Lukashenko aondoke madarakani.

Belarus Proteste in Minsk
Picha: TASS/dpa/picture-alliance

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Belarus ametangaza mgomo wa nchi nzima leo, kuongeza shinikizo kumtaka Rais Alexander Lukashenko aondoke madarakani. Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya maandamano makubwa nchini humo yakutaka kujiuzulu kwa Lukashenko. 

Akitoa wito wa kufanyika mgomo huo, kiongozi mkuu wa upinzani aliye uhamishoni nchini Lithuania , Svetlana Tikhanovskaya amewataka raia wa Belarus kutafakari kuhusu hatma ya watoto wao na kupambana ili kupata haki ya kuwa huru.

Kwenye ujumbe kupitia Telegram aliwataka raia wa Belarus,wasifanye kazi kwa ajili ya Serikali ya Lukashenko. Amesema mgomo kwenye makampuni ya umma itakuwa na shinikizo kubwa ya kiuchumi.

Maandamano mapya mjini Minsk

Swetlana Tichanowskaja - Kiongozi wa upinzani BelarusPicha: Michele Tantussi/Reuters

 Tikhanovskaya amewambia wale wanaohofia kupoteza kazi kubakia nyumbani na kuongeza kuwa yale yanayoendelea yanahitaji ujasiri na ustahamilivu.

 Makumi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, walikusanyika mbele ya vyuo vyao,wakikaa kitako na wengine wakiandamana barabarani.

 Kanda za video zilizotolewa na vyombo vya habari vya upinzani zinaonyesha polisi ikitawanya waandamanaji. Shirika lisilo la serikali la Viasna, linaelezea kwamba zaidi ya watu 100 walikamatwa na polisi mchana wa leo kwenye mji mkuu wa Minsk.

 Shirika huru la utangazaji la Tu.by lilichapisha picha ya makumi ya wafanya kazi kwenye viwanda vikuu vya  umma wakigoma, ikiwemo kwenye kiwanda cha gesi ya kemikali cha Grodnoazot, magharibi mwa nchi.

Serikali ya puuza miito ya kutaka Lukashenko ajiuzulu

Kiongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi wa Belarus, Alexendar Larochouk,amesema kwamba haijulikani hadi lini mgomo huo utadumu kufuatia shinikizo la viongozi dhidi wafanyakazi. Amesema chama chao hakija itisha mgomo huo.

Moja ya wasemaji wa serikali ya Belarus aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba makampuni ya umma yanafanya kazi kama kawaida.

 Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani, ni watu 523 walikamatwa na polisi Jumapili kufuatia maandamano makubwa yaliojumuisha watu zaidi ya laki moja.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wenye utata wa Agosti 9, Belarus inakabiliwa  na wimbi la maandamano ya umma dhidi ya utawala wa miaka 26 wa Rais Lukashenko aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 80.

Vuguvugu la kudai demokrasia linadai kuwa Tikhanovskaya ndiye mshindi wa uchaguzi huo ambao upande wa upinzani unasema uliandamwa na vitendo vya wizi wa kura.