1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavenezuela wamechoshwa na Maduro

2 Agosti 2016

Tume ya uchaguzi ya Venezuela imethibitisha wapinzani wa rais Nicolas Maduro wamekusanya saini za kutosha kuanzisha zoezi la pili la kukusanya sauti kwa lengo la kumng'owa madarakani kiongozi huyo wa kisoshialisti.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Tibisay LucenaPicha: Reuters/C. G. Rawlins

Akizungumzia kupitia televisheni ya nchi hiyo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Venezuela Tibisay Lucena amesema zaidi ya saini laki nne zimetambuliwa,idadi ambayo ni mara dufu ya ile iliyokuwa ikihitajika kuweza kuanzisha zoezi la kumng'owa madarakani rais Maduro.

"Majimbo 24 ya Venezuela yametosheleza asili mia moja ya saini zinazohitajika na uamuzi huu utasajiliwa katika daftari la tume ya uchaguzi."Amesema bibi Tibisay Lucena.

Upande wa upinzani unakabiliwa na kazi ngumu hivi sasa kwasababu zoezi litakalofuata litahusiana na kukusanya saini kutoka asili mia 20 ya wapiga kura au watu milioni nne ili kuyapa nguvu madai ya kutaka kumng'owa rais Maduro madarakani. Ikiwa kura ya maoni itaitishwa,basi rais ataweza kung'olewa madarakani tu ikiwa idadi ya kura za wanaompinga Maduro itapindukia watu milioni saba na laki sita,yaani idadi ya watu waliompigia kura alipochaguliwa kuwa rais mwaka 2013.

Wananchi wa Venezuela wanaona bora Maduro ang'atuke

Katika wakati ambapo matatizo ya kiuchumi yanazidi kuongezeka nchini Venezuela na ughali wa maisha ukizidi kukithiri na mahitaji muhimu yakikosekana,uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha kwamba idadi kubwa ya wananchi wanapendelea Maduro ang'oke madarakani.

Rais Nicolas Maduro wa VenezuelaPicha: Reuters/C. G. Rawlins

Ikiwa wapinzani wa Maduro watafanikiwa katika juhudi zao basi uchaguzi mpya wa rais unaweza kuitishwa haraka. Lakini pindi ukiitishwa mwakani,nafasi ya Maduro inaweza kushikiliwa na makamo wake wa rais na chama chake kuendelea kuwepo madarakani hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa,kama ilivyopangwa mwaka 2018.

Mhula wa Nicolas Maduro unakamilika kimsingi mwaka 2019.

Viongozi wa chama tawala cha kisoshialisti wameshasema hawatoruhusu uchaguzi uitishwe kabla ya mwaka unaokuja.

Upande wa upinzanmi wazidi kutia kishindo

Ndio maana upande wa upinzani unamshinikiza mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Tibisay Lucena atangaze tarehe ya kuanza zoezi la pili na la mwisho kabla ya kura ya maoni.

Wanajeshi wagawa chakula nchini VenezuelaPicha: Reuters/C. G. Rawlins

"Imesalia hatua moja tu kabla ya Venezuela kuingia katika njia ya mustakbal mwema" amesema mbunge wa upande wa upinzani Freddy Guevara kupitia mtandao wa Twitter.

Henriques Capriles,aliyeshindwa chupu chupu na Maduro katika uchaguzi wa rais mwaka 2013,ametoa wito wa kuitishwa maandamano ili kushinikiza zoezi la kumng'owa madarakani rais Maduro liharakishwe.

Nae waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameitolea wito Venezuela isivute wakati katika suala la kuitisha kura ya maoni.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters/AP/dpa/AFP

Mhariri: Josephat Charo