1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wakutana Sri Lanka kujadili serikali mpya

10 Julai 2022

Vyama vya kisiasa vya upinzani nchini Sri Lanka vinakutana Jumapili kukubaliana kuhusu serikali mpya siku moja baada ya rais wa nchi hiyo na Waziri mkuu kutangaza kuachia madaraka

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Picha: Eranga Jayawardena/AP/dpa/picture alliance

Haikubainika kama Rais Gotabaya Rajapka alikuwa katika makaazi yake kwa wakati huo, na msemaji wa serikali Mohan Samaranayake amesema hana taarifa kuhusu aliko.

Soma pia: Rais na Waziri Mkuu Sri Lanka wajiuzulu baada ya maandamano

Mbunge wa upinzani M. A. Sumathiran amesema vyama vyote vya upinzani kwa Pamoja vinaweza kupata kwa urahisi wanacham 113 wanaohitajiaka kuonyesha wingi wa viti bungeni, ambapo kisha watamuomba Rajapaksa kutangaza serikali mpya na kisha kujiuzulu.

Amesema vyama hivyo vinatumai kufikia makubaliano Jumapili. Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe amesema ataondoka madarakani mara baada ya serikali mpya kutangazwa, na saa chache baadae spika wa Bunge akasema Rajapaksa atajiuzulu Jumatano.

Waandamanaji wamesema hawataondoka katika makazi ya rais na waziri mkuu hadi pale viongozi hao watapojiuzulu rasmiPicha: Harendran/DW

Shinikizo dhidi ya viongozi hao wawili lilikuwa limeongezeka baada ya mporomoko wa uchumi kusababisha uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu, na kuwaacha watu wakitatizika kupata chakula, mafuta na mahitaji mengine.

Kama rais na Waziri mkuu watajiuzulu, Spika Mahinda Yapa Abeywardena atachukua usukani kama rais wa muda, kwa mujibu wa katiba.

Waandamanaji walibaki nyumbani kwa Rajapaksa, na kwenye ofisi yake Pamoja na makaazi ya Waziri mkuu, wakisema wataendelea kubaki hapo hadi pale viongozi hao watakapojiondoa rasmi madarakani.

Wanajeshi wamewekwa mjini Colombo na mkuu wa Majeshi Shavendra Silva ametoa wito wa uungwaji mkono wa umma katika kurejesha utulivu.

Rais Gotabaya amesema atajiuzulu ili kurejesha utulivuPicha: Pradeep Dambarage/ZUMA Wire/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema Washington inafuatilia matukio ya Sri Lanka na kulihimiza bunge kufanya kazi haraka kusuluhisha matatizo ya raia. Akizungumza katika kikao cha Habari mjini Bangkok, Blinkena amesema Marekani inakemea mashambulizi dhidi ya waandamanaji wanaoandamana kwa amani na kutoa wito wa uchunguzi kamili katika machafuko yoyote yanayohusiana na maandamano hayo. Sri Lanka inategemea msaada kutoka India na mataifa mengine wakati viongozi wakijaribu kutafuta mpango wa uokozi kutoka kwa IMF. Wickremesinghe amesema hivi karibuni kuwa mazungumzo na IMF yamekuwa magumu kwa sababu Sri Lanka sasa ni taifa lililofilisika.

Nchi hiyo ilitangaza Aprili kuwa inasitisha malipo ya mikopo ya kigeni kutokana na uhaba wa fedha za kigeni. Deni lake la kigeni ni dola bilioni 51, ambapo lazima illipe dola bilioni 28 ifikapo mwisho wa 2027.

Wachambuzi wanasema kuna shaka kama kiongozi yeyote mpya anaweza kwenda mbali Zaidi na alichokifanya Wickremesinghe. Juhudi za serikali yake zilionyesha matumaini, huku mbolea inayohitajika Zaidi ikisambwa kwa wakulima kwa msimu ujao wa kupanda vyakula na shehena ya kwanza ya kesi ya kupikia ikiwasili nchini humo Jumapili.

afp, reuters, dpa, ap