Ukosoaji wa ruhusa ya vyakula vilivyokuzwa kisayansi Kenya
12 Oktoba 2022
Viongozi hao wa Azimio wanasema kuwa, hatua hiyo inalenga kuzinufaisha kampuni za kimataifa, badala ya kuangazia suala la uhaba wa chakula katika taifa hilo ambako watu milioni nne wanakabiliwa na baa la njaa.
Akizungumza alipokuwa akiwahutubia wanachama wa Bunge La Mwananchi katika bustani ya Jevanjee jijini Nairobi, kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga alidai kuwa mbegu zilizokuzwa kwa njia ya kisayansi zinapotumika kwenye mchanga huathiri virutubishi hivyo kupunguza uwezo wa uzalishaji.
Hali ya ukame ya Kenya kwa wakati huu
Hatua ya kuoandoa marufuku hiyo na serikali ya Ruto inatokea wakati majimbo 23 yanapokabiliwa na makali ya kiangazi hivyo kuilazimisha serikali kuingilia kati, huku watu milioni nne wakiathiriwa. Kampuni zinazokuza vyakula hivyo zitafaidi pakubwa, huku wakulima wakilazimika kupunguza bei ya bidhaa zao kwa mujibu wa Raila. "Ujerumani imekataa, nchi ya uholanzi imekataa, Sweden, Ufaransa na Estonia zimekataa. Hayo ni mataifa yote yaliyoendelea kisayansi. Kwa nini yamekataa, kwa sababu wana uhakika yatadhuru maisha ya watu wao.” Alisema Odinga.
Wasiwasi wa vyakula vilivyokuzwa kwa njia ya kisayansi
Kwa upande wake aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka alisema wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki, serikali ilielezea wasiwasi wake kuhusu kuruhusu vyakula vilivyokuzwa kwa njia ya kisayansi kutokana na kitisho cha teknolojia ambacho hakingeathiri tu wakulima nchini lakini pia mazingira. Kalonzo ameaongeza kusema kuwa pana haja ya kuruhusu mjadala wa wadau wote kabla ya kufanya maamuzi.
Taifa la Kenya lilipiga marufuku vyakula vinavyokuzwa kwa njia ya kisayansi mwaka 2012 na kutangazwa na aliyekuwa waziri wa Afya Beth Mugo baada ya jarida moja iliyochapishwa na mwanasayansi wa taifa la Eric Seralini kudai kuwa mimea hiyo ilikuwa na chembechembe za saratani baada ya panya aliyelishwa kupata uvimbe wa saratani.
Soma zaidi:Wakimbizi wa Ethiopia wapewa hifadhi Marsabit
Hata hivyo jarida hilo lilifutiliwa mbali miaka miwili baadaye kwa kutoangazia suala hilo kwa ukamilifu. Musyoka ni anasema kuwa tamko la Rais lina nia mbaya."Kenya haina uwezo wa kutosha wa kufanyia majaribu vyakula vya GMO na athari zake kwa afya, hivyo tunayaweka maisha ya watu wetu katika hatari, kwa kuruhusu GMO nchini.”
Majaribio ya mahindi yaliyokuzwa kwa njia ya kisayansi yalianza kufanyika mwaka 2010, lakini wanasayansi walikamilisha utafiti huo mwaka uliopita na hadi sasa wanasubiri baraza a mawaziri kuyaidhinisha kwa matumizi.
DW, Nairobi