Upinzani wanusa harufu ya ufisadi Zanzibar
31 Julai 2023Tangu Hussein Ali Mwinyi kuingia madarakani kukalia kiti cha urais wa Zanzibar baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, amekuwa akisema kuwa anachukuwa hatua kadhaa za kupambana na ufisadi, lakini viongozi wa chama mshirika katika serikali yake, ACT-Wazalendo, wanamshutumu rais huyo kwa kukiuka sheria na taratibu katika kuendesha nchi na matokeo yake "kuiingiza kwenye miradi yenye harufu ya ufisadi."
Itakumbukwa kuwa wakati anaanza uongozi wake serikalini, Rais Mwinyi alitenguwa na kuteuwa maafisa kadhaa kwa lengo la kuimarisha Taasisi ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), na Ofisi ya Mdhibiti na Msimamizi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG), lakini juhudi zake hizo zinaonekana kufifiya, na badala yake chama cha ACT-Wazalendo kinasema nafasi yake imechukuliwa ubadhirifu unaongezeka kila kukicha.
Shutuma za ufisadi bandari, Uwanja wa Amani
Miongoni mwa yanayolalamikiwa na chama hicho ni hatua ya hivi karibuni ya kuingia mkataba na kampuni binafsi kuendesha bandari ya Zanzibar, ujenzi wa bandari mpya ya Mangapwani, na ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Amani.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kati kisiwani Unguja siku ya Jumapili (Julai 30), Mjumbe wa Kamati Kuu wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa, alisema kuna kiwango kikubwa cha kudharau sheria za manunuzi na utoaji zabuni kwenye miradi unaofanyika bila ya kuwepo uwazi.
Makamo Mwenyekiti wa chama hicho na ambaye pia ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisema rasilimali za nchi zilizopo ni mali ya wananchi na kwamba kila kiongozi "mwenye dhamana anawajibika kuzisimamia kwa uwazi, uaminifu na uadilifu ili kuleta maendeleo kwa niaba ya wananchi wenyewe."
Rais Mwinyi atetea maamuzi ya serikali
Katika mkutano wake na waandishi habari hivi karibuni, Rais Mwinyi alisema mikataba inayoingiwa na utawala wake inazingatia maslahi ya nchi, na alipuuzia kabisa madai ya ufisadi, ukiukwaji wa sheria na ukosefu wa uwazi.
Kama ilivyo kwa masuala yoyote yanayohusu serikali, hata hili nalo linaonekana kuwagawa wananchi wa Zanzibar kwa misingi ya vyama vyao. Wakati wafuasi wa chama tawala, CCM, wakiunga mkono kila hatua inayochukuliwa na serikali ya Rais Mwinyi, wale wanaoelemea upinzani wanasikitishwa na ubadhifu unaofanyika na kuamini kwamba baadhi ya watendaji hushindwa kumshauri vyema Rais wa nchi.
Imetayarishwa na Salma Said/DW Zanzibar