Upinzani wazidi mkataba wa madini wa Kongo-Marekani
11 Februari 2026
Upinzani dhidi ya mpango wa kuruhusu kampuni za Marekani kupata madini muhimu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaongezeka, baada ya Rais Felix Tshisekedi kurejea kutoka mkutano wa madini uliofanyika Marekani wiki iliyopita.
Ziara hiyo ilimpatia sifa kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na baadhi ya wabunge wa Marekani.
Tshisekedi ameahidi kufungua milango kwa kampuni za Marekani kuwekeza katika madini ya mashariki mwa Kongo, ambayo bado hayajachimbwa kikamilifu na yanakadiriwa kuwa na thamani ya dola trilioni 24.
Hatua hiyo inachukuliwa kama karata ya mazungumzo ili kupata msaada wa Marekani katika kukabiliana na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda na katika kujenga miundombinu muhimu katika eneo hilo.
Mpango huu unakuja wakati utawala wa Trump unatafuta kuunda muungano wa biashara ya madini na washirika wake, ili kupunguza utegemezi wa dunia kwa China katika sekta ya madini adimu.
China inachangia karibu asilimia 70 ya uchimbaji wa madini adimu duniani na inadhibiti karibu asilimia 90 ya usindikaji wake. Aidha, China ndiyo mwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya madini ya Kongo.
Ushindani wa Marekani na China waongezeka
Marekani na Kongo zinasema ushirikiano wao wa kimkakati utasaidia kulinda mnyororo wa usambazaji wa madini muhimu kama cobalt, shaba, lithiamu na coltan. Kwa upande wa Kongo, inatarajiwa kupata msaada wa maendeleo ya miundombinu na usalama.
Hata hivyo, wachambuzi na wakazi wa Kongo wanasema bado hakuna dalili kwamba ushiriki wa Marekani utaleta amani ya kudumu, hasa mashariki ambako waasi wa M23 wanadhibiti maeneo yenye madini mengi, ikiwemo mgodi wa Rubaya unaozalisha takriban asilimia 15 ya coltan duniani.
Hivi karibuni, wachimbaji wasiopungua 200 walifariki baada ya sehemu ya mgodi huo kuporomoka.
Mtafiti Josaphat Musamba wa Chuo Kikuu cha Ghent nchini Ubelgiji anasema ushindani kati ya China na Marekani "utaongezeka kwa nguvu katika ardhi ya Kongo.”
Hofu za kupoteza uhuru wa taifa
Katika mji mkuu Kinshasa, viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kiraia wanapinga makubaliano hayo wakisema yanaweza kuathiri uhuru wa taifa. Kundi la mawakili na watetezi wa haki za binadamu limewasilisha kesi mahakamani likidai mkataba huo unatishia mamlaka ya Kongo juu ya rasilimali zake.
Wakili Jean-Marie Kalonji amesema wanachukua hatua hiyo kulinda urithi wa taifa kwa vizazi vijavyo.
Kiongozi wa upinzani Moïse Katumbi pia amehoji jinsi mkataba huo utakavyotekelezwa katika mazingira ya ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi. Ameitaka serikali kuanzisha mazungumzo ya kitaifa kabla ya kuingia mikataba mikubwa ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu Fulgence Muteba wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kongo amefananisha ushirikiano huo na "kuuza madini ya taifa zima ili kuokoa utawala wa kisiasa.”
Katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, baadhi ya wakazi wanasema hawaoni dhamira ya wazi ya Marekani kurejesha amani. Mwanaharakati wa vijana Christopher Muyisa anahofia kuwa makubaliano hayo yanaweza kuzua migogoro zaidi badala ya kutoa suluhisho.
Kwa mujibu wa mchambuzi Yvon Muya wa Chuo Kikuu cha Ottawa nchini Canada, faida ya haraka kwa Tshisekedi ni ya kisiasa — kupata utambuzi wa kimkakati kutoka Washington.
Hata hivyo, swali kubwa ni kama makubaliano hayo yataleta maendeleo na amani kwawananchi wa Kongo, au yataongeza tu ushindani wa kimataifa juu ya ardhi yao yenye utajiri mkubwa wa madini.