Upinzani wapinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa Kongo
3 Desemba 2011Chama hicho cha Etienne Tshisekedi, kimeilaumu Tume cha Uchaguzi kwa kufanya uchokozi wa makusudi, kwa kuchagua kutangaza matokeo katika maeneo machache tu, ambayo Kabila ameshinda. Katibu Mkuu wa chama hicho, Jacquemin Shabani, amesema tume imetangaza matokeo ya asilimia 0.2 ya vituo, ilhali zaidi ya matokeo ya asilimia 90 ya vituo yameshakusanywa.
Katika matokeo hayo ya awali, Rais Kabila anaongoza dhidi ya Tshisekedi. Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa jana, karibu asilimia 15 ya kura zilizohesabiwa zinaonesha Kabila anaongoza kwa zaidi ya kura milioni moja na nusu, ambayo ni takriban asilimia 52. Tshisekedi, ambaye ni miongoni mwa wagombea 11, ameshika nafasi ya pili kwa kupata 997,074, sawa na asilimia 34.
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, Daniel Ngoy Mulunda, ametoa matokeo hayo ya awali ikiwa ni siku nne baada ya kufanyika uchaguzi Jumatatu iliyopita.