Upinzani wataka mazungumzo ya Geneva yaharakishwe
18 Machi 2016Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria, Staffan de Mistura, alisema pengo kati ya serikali ya Syria na upinzani ni kubwa lakini wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuiweka Syria pamoja na kuukataa mfumo wa shirikisho.
De Mistura aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hali nchini Syria imekuwa ya utulivu katika siku tatu zilizopita baada ya karibu wiki tatu za usitishwaji uhasama, lakini akatahadharisha kuna umuhimu wa kuendelea kuwa macho, kwa kuwa mambo yanaweza kubadilika haraka sana.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alisema alifanya mazungumzo ya maana na Kamati Kuu ya mazungumzo ya Syria, HNC, na mapendekezo yaliyowasilishwa yalikuwa ya kina. "Leo jioni hii tumefanya mkutano wa maana na baraza la upinzani HNC. Watakuja kunifuatilia kwa kauli zao wenyewe. Yalikuwa mazungumzo ya kina. Makaratasi kuhusu mpito wa kisiasa yalisambazwa na walijadili kwa kina vipi wanavyoona kipindi hiki cha mpito kinavyoweza kutekelezwa hivi karibuni."
Kuhusu suala la wafungwa De Mistura alisema ingawa pande zote mbili husika katika mzozo wa Syria zinawazuilia wafungwa, idadi ni kubwa mno kwa upande wa serikali. Awali mshauri wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinaadamu, Jan Egeland, alisema ana matumaini ya kupata ufanisi katika juhudi za kuachiwa wafungwa, hususan wanawake, watoto na wagonjwa. Egeland alizitolea wito Marekani na Urusi na nchi nyingine zizishinikize pande zote za Syria.
Upinzani wataka kupiga hatua haraka
Upinzani wa Syria ulisema ungependelea kupiga hatua haraka chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuwa na kipindi cha mpito nchini humo. Akizungumza baada ya mkutano kati ya kamati kuu ya majadiliano, HNC, na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria, Staffan de Mistura, mwanachama wa kamati hiyo, Bassma Kodmani, alisema wamewasilisha waraka kuhusu mtizamo wao wa kipindi cha mpito na kuundwa kwa chombo cha mpito kitakachoingoza Syria.
"Tunataka kwenda haraka, tunataka kuepuka mchakato ambao hauzai matunda. Bwana de Mistura amesisitiza kuna muda wa miezi sita, kwa matumaini pengine uwe chini ya miezi sita, lakini hautapita. Na hilo kwetu sisi ni hakikisho muhimu," aliongeza kusema Kodmani.
Alipoulizwa kuhusu kucheleweshwa kwa mazungumzo kunakoweza kusababishwa na ujumbe wa serikali, Kodmani alisema wao wapo Geneva na wanatumai Umoja wa Mataifa utalishughulikia suala hilo. Kodmani aidha alisema wanauchukulia mchakato wa Geneva kuwa wa umuhimu mkubwa na ni jukumu la de Mistura kuhakikisha unafaulu.
Mwandishi:Josephat Charo/afp/rtre
Mhariri:Yusuf Saumu