Upinzani Senegal waapa kupinga kuahirishwa uchaguzi
8 Februari 2024Wiki chache kabla ya uchaguzi wa urais wa Februari 25 kufanyika, bunge la Senegal mnamo siku ya Jumatatu lilipiga kurakuunga mkono tangazo la Rais Macky Sallla kuahirisha uchaguzi hadi Desemba. Tangazo hilo lilichochea wasiwasi wa kimataifa na hasira kubwa ya umma ndani ya taifa hilo.
Takribani wagombea 12 kati ya 20 waliopitishwa kuwania urais, wameafikiana kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi. Anta Babacar anayekiongoza chama cha Alternative for the Next Generation of Citizens ARC, amesema kuwa wanapanga kuliwasilisha shauri hilo katika mahakama ya juu na kufanya maandamano makubwa.
"Hii haihusu chama cha kisiasa. Tumeamua kuondoa rangi za vyama vyetu. Kuna rangi moja tu nayo ni Senegal. Tunalo lengo moja sasa. Ni kuhakikisha kuwa rais Macky sall hatekelezi mamlaka yake ya muhula wa tatu. Na tunaelekea kwenye uchaguzi," amesema mgombea huyo Anta Babacar.
Sall, ambaye amefikia ukomo wa kikatiba wa mihula miwili madarakani, alisema kwamba kuahirishwa kwa kura hiyo kunatokana na mgogoro wa orodha ya wagombea na ufisadi ndani ya tume ya uchaguzi.
Hayo yakijiri, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, wanafanya kikao cha dharura leo, huku ajenda kuu ni mkwamo wa kisiasa wa Senegal na mizozo baina ya jumuiya hiyo na viongozi wa kijeshi katika mataifa matatu yaliyokumbwa na mapinduzi.
Kulingana na Baraza la usuluhishi na usalama la ECOWAS, mawaziri hao wanakutana katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja, kujadili masuala ya kiusalama na kisiasa ya kikanda. Hata hivyo haikuwekwa wazi ikiwa Senegal itawakilishwa na waziri yeyote.
Tangazo la Sall: Rais wa Senegal ahairisha uchauzi wa februari katika kipindi kisichojulikana
Jumuiya hiyo ya ECOWAS imeirai Senegal, moja ya wanachama wake thabiti, kurejea katika kalenda ya uchaguzi, lakini wakosoaji tayari wametilia shaka mwelekeo wa muungano huo kutokana na ongezeko la wanachama wanaozidi kukaidi.
Mkwamo huo wa kisiasa wa Senegal pia umetilia shaka umuhimu wa jumuiya hiyo yenye umri wa miaka 50, hasa baada ya onyo lake la kuingilia kati kijeshi nchini Niger kutofanikiwa.
Ghasia: Vurumai yazuka baada ya bunge la Senegal kuahirisha uchaguzi wa rais
Nao Umoja wa Ulaya umeeleza kwamba uamuzi wa hivi karibuni wa kuahirisha uchaguzi wa Senegal "unatia doa mafanikio ya muda mrefu ya demokrasia" nchini humo na unapaswa kubatilishwa.
Matamshi ya Umoja wa Ulaya yaliyotolewa jana, yameunga mkono ukosoaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani ambayo ilisema kuwa kura ya hivi karibuni ya kuahirisha uchaguzi "haiwezi kuchukuliwa kuwa ni halali".
Vyanzo: AFP/Reuters