1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Upinzani Zimbabwe waenda mahakamani baada ya zuio la mkutano

8 Julai 2023

Chama kikuu cha upinzani cha Zimbabwe cha "Citizen Coalition for Change" (CCC) kimekwenda mahakamani leo, kupinga uamuzi wa polisi wa kuzuia mkutano wao wa hadhara uliopangwa Jumapili.

Rasi Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe
Rasi Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe Picha: Jekesai Njikizana/AFP/Getty Images

Chama hichoo kilizuiwa kufanya mkutano huo katika mji wa Bindura kaskazini mwa mji mkuu Harare kwa kile polisi ilichosema kuwa, mahali wanakotaka kuufanya kusanyiko hilo hapafai kwani ni "porini" na barabara zake "hazifai kutumika."

Chama hicho kikuu cha upinzani cha Zimbabwe kimesema hatua ya kupigwa marufuku kwa mkutano wao ni mfano mwingine wa namna utawala wa Rais Emmerson Mnangagwa unavyokandamiza vyama vya upinzani kabla ya uchaguzi wa Agosti 23.

Mbali na chama hicho, makundi huru ya haki za binadamu yamekuwa yakiituhumu serikali ya Rais Mnangagwa kwa kuuonea upinzani kwa kuwakamata maafisa na wafuasi wake na kuzuia mikutano karibu na uchaguzi wakati wafuasi wa chama tawala wakifanya vurugu ili kuwatisha wenzao wa upinzani.