1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Upinzani Zimbabwe wapinga ushindi wa Mnangagwa

28 Agosti 2023

Upinzani nchini Zimbabwe umeyapinga matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyomrejesha madarakani rais Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF.

Simbabwe I Politik I Nelson Chamisa
Wafuasi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Citizens Coalition for Change (CCC) Picha: Zinyange Auntony/AFP/ Getty Images

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Citizens Coalition for Change (CCC) kimetangaza msimamo wa kuyapinga matokeo hayo ya uchaguzi mnamo Jumapili siku moja ya baada ya Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo kumtangaza rais Mnangagwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Jumatano iliyopita.

Matokeo ya tume yameonesha kiongozi huyo wa chama cha ZANU-PF alishinda muhula mwingine madarakani kwa kupata asilimia 52.6 ya kura dhidi ya mwanasiasa machachari wa upinzani Nelson Chamisa aliyejikingia asilimia 45.

Upinzani umesema hauyatambui matokeo hayo ya uchaguzi wanaodai ulijaa "hila na udanganyifu usio kifani".

Chimasa asema watayapinga matokeo kwa nguvu kubwa

Kiongozi wa upinzani wa chama cha Citizens Coalition for Change (CCC) nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa Picha: KB MPOFU/REUTERS

Katika tamko la kwanza tangu kutolewa matokeo hayo, Chamisa aliandika matamshi makali ya kuyapinga upitia ukurasa wa mtandao X uliofahamika zamani kama Twitter.

Amesema matokeo ya uchaguzi huo yamechakachuliwa na wananuwia kuyapinga kisheria china ya msingi kuwa "zoezi la kuheshabu na kuyajumlisha halikufanyika kwa usahihi".

Sehemu ya ujumbe wa Chamisa inasema na hapa ninanukuu "wameiba sauti na na kura zenu lakini kamwe siyo matumaini yenu" mwisho wa kunukuu.

Baadae kidogo kulikuwa na mkutano kati ya chama hicho na waandishi habari mjini Harare ambapo Chamisa alirejea madai yake ya wizi wa kura na kuapa kuwa upinzani hautanyamaza.

"Mabadiliko yanakuja Zimbabwe, iwe chama cha ZANU-PF kinayataka au hakiyataki. Haitokuwa rahisi lakini mabadiliko yanakuja. Hatutasubiri miaka mingine mitano, mabadiliko lazima yatokee sasa na tutakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mabadiliko yanatokea Zimbabwe.Ni lazima tukomeshe uwendawazimu huu", amesema Chamisa

Rais Mnangagwa awataka wanaopinga matokeo waende mahakamani 

Emmerson Mnangagwa ametangazwa mshindi wa muhula mwingine madarakani katika uchaguzi wa Agosti 23Picha: Jekesai Njikizana/AFP via Getty Images

Haijafahamika mara moja ni vipi Chamisa analenga kutimiza lengo hilo la mabadiliko lakini mpinzani wake aliyetangazwa mshindi rais Emmerson Mnangagwa aliwakosoa wanaoyapinga matokeo ya uchaguzi na kuwakumbusha wanayo haki ya kwenda mahakamani.

Katika ujumbe aloutoa baada ya kutolewa matokeo Mnangagwa aliusifu uchaguzi huo kuwa wa kihistoria na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika muhula mpya wa utawala wake.

"Hakuna washindi na walioshindwa, lakini kuna taifa moja tu la watu wa Zimbabwe walioungana. Kwa jumla tumewaabisha wabaya wetu waliotamani kutuona tunagawika na kutumbukia kwenye machafuko. Daima tutabakia wamoja, wapenda amani na watu wastahamilivu", amesisitiza Mnangagwa.

Waangalizi watilia shaka viwango vya uchaguzi wa Zimbabwe 

Wanaagalizi wa kimataifa ikiwemo Jumuiya ya kikanda ya SADC wamesema uchaguzi wa Zimbabwe ulikuwa na dosari.Picha: Shaun Jusa/Xinhua/picture alliance

Licha ya msisitizo huo wa rais Mnangagwa uchaguzi huo wa rais na bunge ulishuhudia dosari kadhaa siku ya yenyewe ya upigaji kura.

Kulikuwa na ucheleweshaji kufunguliwa vituo vya kupigia kura na hata kile kimetajwa kuwa ukandamizaji wa wapiga kura.

Katika baadhi ya wilaya uchaguzi ulilazimika kufanyika siku iliyofuata.

Changamoto hizo ndiyo zimefanya timu za waangalizi wa kikanda na kimataifa kuhitimisha kuwa uchaguzi wa Zimbabwe haukukidhi viwango vya kimataifa.

Ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, ni miongoni mwa taasisi zilizotoa tathmini ya aina hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress naye alizungumzia mashaka yake baada ya kuwepo taarifa za kukamatwa kwa waangalizi, vitisho kwa upinzani na wapigakura.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW