1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uporaji na vurugu zazidi kutanda Afrika Kusini

14 Julai 2021

Idadi ya watu waliofariki nchini Afrika Kusini karika maandamano ya vurugu imeongezeka na kufikia zaidi ya 70.

Schwere Unruhen in Südafrika nach Verurteilung von Ex-Präsident Zuma
Picha: Rogan Ward/Reuters

Maandamano hayo yaliyochochewa na hatua ya kufungwa jela kwa rais wa zamani Jacob Zuma, yamedumu kwa muda wa wiki moja sasa. Pia yamekumbwa na visa vya uporaji mali, vurugu na biashara kufungwa. 

Maandamano hayo yalianza wiki iliyopita baada ya rais wa zamani Jacob Zuma kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 jela. Zuma alihukumiwa kwa kukaidi agizo la mahakama, la kumtaka afike mahakamani katika kesi ya rushwa dhidi yake.

Maandamano hayo yametanuka na kukumbwa na vurugu, waandamanaji wakiyapora maduka na kuonyesha ghadhabu zao kutokana na ugumu wa maisha na ukosefu wa usawa miongoni mwa watu wa tabaka mbalimbali miaka 27 tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Maduka pamoja na mabohari yameporwa au kuchomwa moto, hasa katika mkoa wa nyumbani kwa Zuma, KwaZulu Natal, katika mji mkuu Johannesburg na katika viunga vya mkoa wa Gauteng.

Polisi yatoa onyo kwa waporaji

Baadhi ya waandamanaji wakipora maduka mjini Johannesburg.Picha: Sumaya Hisham/REUTERS

Polisi imesema kwenye taarifa kwamba vurugu hizo zilienea katika mikoa mingine miwili usiku wa kuamkia leo Mpumalanga na Nothern Cape. 

"Hakuna kiwango chochote cha kutoridhishwa na jambo au hali yoyote isiyopendeza humpa mtu haki ya kupora, kuharibu na kufanya watakavyo huku wakivunja sheria. Tunatoa wito kwa jamii kujizuia na zaidi ya yote ihakikishe raia hawajeruhiwi. Tunatoa wito zaidi kwa watu na makundi kukataa wito wowote wa kufanya vurugu na kufanya nchi ikose utulivu," amesema Bheki Cele.

Vituo vya televisheni nchini humo vimeonesha uporaji zaidi wa maduka ukiendelea leo katika mji wa Soweto na mji wa bandari wa Durban.

Afisa mmoja wa sekta ya viwanda amesema kiwanda kikubwa zaidi cha mafuta nchini Afrika Kusini SAPREF kilichoko Durban kimefungwa kwa muda kufuatia ghasia zinazoendelea.

Umoja wa Mataifa Afrika Kusini waeleza wasiwasi

Maandamano ya vurugu Afrika Kusini yamechochewa na kufungwa jela kwa rais wa zamani nchini humo.Picha: Rogan Ward/REUTERS

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Afrika Kusini imeelezea wasiwasi kwamba maandamano hayo ya vurugu yametatiza usafiri kwa wafanyakazi, wahudumu wa afya na pia yanasababisha upungufu wa vyakula, dawa na bidhaa nyingine muhimu.

Kwenye taarifa, Umoja wa Mataifa nchini Afrika Kusini umeongeza kuwa hali iliyoko inazidisha hali duni za kijamii na kiuchumi ambazo zimekuwepo kutokana na ukosefu wa nafasi za ajira, umaskini na ukosefu wa usawa nchini humo.

Mnamo Jumanne, wanajeshi walipelekwa mitaani kuwasaidia polisi ambao walishalemewa kujaribu kudhibiti machafuko. Mamlaka ya mashtaka ya umma imesema itawaadhibu wale watakaokamatwa wakipora na kuharibu mali. Lakini onyo hilo halijazuia uporaji au uharibifu unaoshuhudiwa.

Jacob Zuma ambaye ana umri wa miaka 79 kwa sasa, ni rais wa zamani wa Afrika Kusini, mpiganaji wa zamani katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi. Aliwahi kufungwa jela miaka 10 katika gereza lenye sifa mbaya kisiwani Robben karibu na mji wa Capetown.

Licha ya kesi za ufisadi kumuandama, angali maarufu miongoni mwa raia wengi maskini nchini Afrika kusini hususan wafuasi wa chama tawala ANC vijijini.

(RTRE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW