1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Ukoloni wa Ujerumani

21 Desemba 2023

Kufikia mwaka 1885, Adolf Lüderitz alishajipatia maeneo makubwa ndani ya Namibia ya leo. Lakini mikataba yake na wenyeji ilikuwa na utata kiasi cha kwamba hata maafisa wa ukoloni wa Ujerumani waliitilia shaka.

Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatengenezwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatengenezwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Vipi Ujerumani ilipata udhibiti wa Namibia ya sasa?

Kufikia miaka ya 1880, wachora ramani wa Ulaya walijuwa kulikuwa na ghuba tatu tu salama kwa meli kutia nanga kwenye mwambao wa takribani kilomita 2,000 (maili 1,242). Waliposhuka, wasafiri walikutana na jangwa tupu lenye ukubwa wa kilomita 140 kuelekea ndani: Jangwa la Namib.

Chifu wa Wanama, Josef Fredericks II, alimpokea mfanyabiashara kijana wa Kijerumani aliyeitwa Heinrich Vogelsang katika eneo la Bethany kusini mwa Namibia mwaka 1883.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Pili

This browser does not support the audio element.


Kwa niaba ya mfanyabiashara wa Kijerumani, Adolf Lüderitz, Vogelsang alimzawadia Fredericks bunduki 200 na paundi 100 kwa ajili ya eneo linalozunguka ghuba moja tupu kwenye mwambao wa Atlantiki. Miezi michache baadaye, mkataba mwengine ukafuatia: bunduki 60 na paundi 500 kwa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa meli za kijiografia 20 kuingia ndani na eneo lote la kusini kuelekea Mto Orange, mpakani mwa Afrika Kusini.

Kwa nini manunuzi haya ya ardhi yana utata?

Kipimo cha wenyeji kilikuwa maili za Muingereza, ama kilomita 1.6 kwa wakati huo. Meli za kijiografia zilikuwa hazijafahamika wakati huo - na hicho ndicho kiini chenyewe. Kwa sababu meli za kijiografia za Ujerumani ambazo mfanyabiashara huyo alikuwa akikusudia ni sawa na kilomita 7.4. Hiyo ni karibuni mara sita zaidi!

Lüderitz, Vogelsang, na wamishionari walioshuhudia manunuzi haya walijuwa kuwa Fredericks hakuwa akijuwa kiwango gani cha ardhi ya watu wake alikuwa akiiuza.

Vipi ardhi iliyonunuliwa na mtu binafsi Afrika ilikuwa sehemu ya dola la Ujerumani?

Ardhi zilizopatikana na raia wa Ujerumani katika nchi za Kameruni, Afrika Kusini Magharibi na Afrika Mashariki baadaye zilichukuliwa na serikali ya Ujerumani.

Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"

Kwenye ramani za kikoloni, kulionekana nchi iitwayo Lüderitzland, na mwezi Agosti 1884, Ujerumani iliitangaza Lüderitzland kuwa mahamiya. Hili liliashiria hatua muhimu kwa malengo ya Ujerumani ya kuunda koloni la walowezi.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

02:47

This browser does not support the video element.


Lüderitz alikuwa ametazamia kupata utajiri mkubwa kwa kununua ya ardhi kwenye Jangwa la Namib kupitia kutafuta na kuchimba madini kama vile shaba. Kuna wakati alimiliki mwambao wote wa Namibia ya sasa. Bahati mbaya, hakugunduwa chochote na akamalizikiwa na pesa.

Lüderitz aliuza mali zake zote kwa Jumuiya ya Makoloni ya Ujerumani mwaka 1885 na akapotelea kwenye misafara muda mchache baadaye.

Wapi kwengine mikataba ilitumika kupata ardhi?

Mikataba iliyosainiwa kote barani Afrika haikuwa ikifahamika kikamilifu na wenyeji, haikuwa ikichukuliwa kwa umakini, ama ilikubalika kwa misingi ya kudanganyana. Nchini Kameruni, maafisa wa Kijerumani walifika umbali wa kufuta na kudharau kabisa matakwa ya machifu kwenye Mkataba wa Germano Douala wa mwaka 1884.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

01:59

This browser does not support the video element.



Mwishoni mwa mwaka 1884, Carl Peters, bila ya hata kupata ruhusa ya moja kwa moja kutoka serikali ya Ujerumani, alitembea kwenye Tanzania Bara ya sasa, akiwasaka machifu kuwataka wasaini nyaraka alizoziandika kwa lugha ya Kijerumani. Mara nyingi, baada ya kupewa ulevi, machifu hao waliahidiwa ulinzi wa Ujerumani.

Kwa nini serikali ya Ujerumani inayatambuwa madai haya?

Ni vigumu kuamini kwamba mtu kama Kansela Otto von Bismarck, ambaye awali alikuwa na mashaka na Ujerumani kuchukuwa makoloni, angelikuja baadaye kuifurahikia mipango ya wafanyabiashara wenye tamaa kama Carl Peters, Adolf Lüderitz, au Adolph Woermann.

Lakini katikati ya miaka 1880, mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiwania makoloni barani Afrika. Peters, kwa mfano, alijenga hoja kwamba maslahi ya Ubelgiji katika Afrika ya Kati yangeliweza kuathiri malengo ya Ujerumani. Bismarck alizidiwa na shinikizo la kisiasa na akakubali kuyapa 'maeneo' ya Peters hadhi ya kuwa 'mahamiya.'

Ipi ilikuwa dhamira hasa ya "mahamiya"?

Kile kilichoitwa "mikataba ya mahamiya" ilisainiwa kimagube kutowa ulinzi wa Ujerumani kwa wenyeji waliosaini madhali tu wamejisamilisha kwa Ujerumani. Katika uhalisia, ilikuwa inarasimisha madai ya ukoloni wa Berlin dhidi ya mataifa mengine washindani ya Ulaya na ilimaanisha kuwa serikali ya Ujerumani ingelizilinda miliki hizi. Kwa hivyo, ilikuwa ni msingi wa mataifa mengine ya Ulaya kuheshimu mikataba hiyo, lakini lilipokuja suala la kuiheshimu mikataba hiyo na Waafrika, mikataba hiyo iliyosainiwa na Wajerumani mara nyingi haikuwa ya ukweli na ilikuwa ya mashaka.

Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani inatengenezwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Soma zaidi: Kampuni ya Woermann ilivyousafirisha ukoloni wa Ujerumani

Mikataba ya mahamiya ilizipa kampuni za Kijerumani fursa ya kutumia ardhi, rasilimali, na nguvu kazi rahisi na iliziruhusu kuleta wanajeshi wa Kijerumani pamoja na silaha.

Kwa nini viongozi wa wenyeji walisaini mikataba kama hiyo?

Inatia mashaka kwamba viongozi wa wenyeji nchini Tanzania, Namibia, Togo au Kameruni walikuwa wakielewa walichokuwa wanakisaini. Machifu wengine walitaka silaha za kupambana na mahasimu wao. Wengine, kama machifu wa Douala nchini Kameruni, walishuhudia matakwa yao yakifutwa kwenye nakala ya Kijerumani ya mkataba, na katika matukio mengine, wakoloni wa Kijerumani, wakijuwa kuwa wanaungwa mkono na silaha nzito nzito na jeshi lenye utaalamu, waliyadharau kwa makusudi makubaliano hayo.

Yapi yalikuwa matokeo kwa wenyeji?

Uendeshaji wa makoloni ulikuwa mikononi  mwa wakoloni wachache wa Kijerumani. Hakuna aliyekuwa akipigania maslahi ya wenyeji, na mara nyingi walitumia nguvu za kijeshi kuangamiza upinzani, na kupata wafanyakazi kwenye miradi ya miundombinu na mashamba.

Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani inatengenezwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW