Urais Kenya-Raila aungana na Kalonzo
4 Desemba 2012Huu utakuwa muungano wa pili kabla ya tarehe ya mwisho (04-12-2012) iliyowekwa na msajiri wa vyama vya siasa iliyotaka vyama hivyo viwe vimekamilisha taratibu za kisheria za muungano wa vya muungano wao katika siku tisini.
Watuhumiwa wa ICC waungana
Awali jumapili (02-12-2012) wanasiasa wawili wa Kenya ambao wanawania wadhifa wa urais na ambao wameshtakiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa kuhusika na uchochezi wa ghasia baada ya uchaguzi, walisema kuwa watajiunga pamoja katika uchaguzi mkuu mwakani wakiwa wagombea wenza wa kiti hicho.
Makamu waziri mkuu Uhuru Kenyatta, mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya baada ya uhuru kutoka Uingereza, atawania kiti cha urais wakati waziri wa zamani William Ruto anamatumaini ya kuwa makamu rais, kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza chini ya katiba mpya na wa kwanza tangu uchaguzi wa mwaka 2007 ambao umesababisha ghasia na zaidi ya watu 1,200 wameuwawa. Kenya hapo kabla imekuwa pepo ya utulivu katika eneo ambalo limekuwa likikumbwa na matatizo.
Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague imesema mwezi Julai kuwa wakenya wanne maarufu , ikiwa ni pamoja na Kenyatta na Ruto, wanahukumiwa kwa madai ya kuhusika katika uchochezi wa ghasia zilizosababisha umwagikaji wa damu. Wote wanakana madai hayo.
Hofu ya mkwamo wa kisiasa Kenya
Kuna hofu kuwa Kenya inaweza kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa ama vikwazo vya kiuchumi kutoka mataifa ya magharibi iwapo watu hao watakaidi kufika katika mahakama ya ICC. "Tumekubaliana kuwa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, mwaka ujao chama cha URP na TNA vitaungana na kuunda serikali mpya," Ruto aliwaambia maelfu ya wafuasi wao katika mkutano wa hadhara wa makundi hayo ya United Republican Party na National Alliance Party cha Kenyatta katika mji wa Nakuru katika jimbo la Rift Valley, kilometa 140 kaskazini magharibi ya mji mkuu Nairobi.
Mawaziri wanane na wabunge kadha walikuwapo katika mkutano huo.
Mahakama ya ICC imepanga kesi hizo za uhalifu dhidi ya ubinadamu zisikilizwe mwezi Aprili , mwakani , mwezi mmoja baada ya uchaguzi wa rais katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika Afrika mashariki.
Hatua ya Ruto na Kenyatta kuungana kuwania urais nchini Kenya , inaleta uwezekano wa kuwa na rais ambaye ameshtakiwa katika mahakama ya ICC mjini The Hague.
Shrika la kijamii nchini Kenya linalojulikana kama International Centre for peace and conflict, taasisi inayoshughulikia uchunguzi wa amani na mizozo imefungua mashtaka siku ya Ijumaa katika mahakama kuu ya kenya kupinga uwezekano wa Ruto na Kenyatta kuwania madaraka ya kuchaguliwa, kutokana na kesi yao mjini The Hague. Kesi hiyo imefunguliwa baada ya kesi kama hiyo kuondolewa mahakamani.
Uchunguzi wa maoni mwezi Oktoba yameonyesha kuwa karibu robo ya Wakenya wanatarajia uchaguzi wa rais mwezi Machi kuchafuliwa na ghasia za baada ya uchaguzi huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu