1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urais wa Hungary utaimarisha au kuudhoofisha Umoja wa Ulaya?

Sylvia Mwehozi
24 Juni 2024

Hungary itachukua urais wa kupokezana wa baraza la Umoja wa Ulaya mnamo Julai mosi, huku kukiwa na uwezekano wa athari katika sera ya Ukraine na mabadiliko ya tabia nchi. Hilo litaleta mabadiliko gani?

Hungary | Umoja wa Ulaya | Urais wa EU
Hungary imesema urais wake wa Umoja wa Ulaya utaongozwa na kaulimbiu ya "Kuifanya Ulaya kuwa kanda kubwa kwa mara nyingine" Picha: Peter Lakatos/EPA

Haikuwa suala la kushangaza wakati Hungary ilipoweka wazi kauli mbiu yake mapema wiki iliyopita yenye maneno ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika kipindi chake cha uongozi wa miezi sita cha urais wa baraza la Umoja wa Ulaya.

Maneno hayo ya "Ifanye ulaya kuwa kubwa zaidi" yalizusha wasiwasi kwa baadhi ya nyuso mjini Brussels.

Kiongozi wa siasa za kizalendo na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ni mkosoaji mkubwa wa Umoja wa Ulaya.

Katika muongo mmoja uliopita, serikali yake imezozana na maafisa wa Umoja wa Ulaya na nchi nyingine wanachama kuhusu kushuka kwa demokrasia nchini mwake, masuala ya wahamiaji na hivi karibuni kuhusu msaada wa kijeshi wa nchi hiyo kwa Ukraine.

Budapest mara kwa mara imetumia kura yake ya turufu katika kura muhimu, na kukwamisha baadhi ya sera wakati nchi nyingine zikiwa tayari kuendelea. Urais wa Baraza la Umoja wa Ulaya ni uongozi wa kupokezana wa miezi sita ambao hupitishwa kati ya nchi 27 wanachama.

Mashaka tayari yameanza kujitokeza kuhusu urais wa Hungary

Waziri Mkuu wa Hungary Victor Orban.Picha: Attila Volgyi/Xinhua/IMAGO

Mnamo Juni mwezi uliopita, wabunge wengi wa Umoja wa Ulaya walipitisha azimio linalohoji "vipi Hungary itaweza kutekeleza kikamilifu jukumu lake mwaka 2024, kwa kuzingatia kuwa inakiuka sheria za muungano huo."

Lakini azimio hili lisilo na nguvu kisheria halikufika mbali. Mnamo Julai mosi, Hungary itaanza kuongoza mikutano katika ngazi ya wizara na ile ya kilele, ikichukua kijiti kutoka kwa Ubelgiji.

Hadi mwisho wa mwaka, itawakilisha pia mataifa mengine wanachama katika mazungumzo ya Bunge na Tume ya Ulaya.

Siku ya Jumanne wiki iliyopita katika mkutano na waandishi wa habari mjini Budapest, waziri wa Hungary anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Janos Boka aliapa kuwa nchi yake itafanya kazi kwa tija.

"Katika kipindi chetu cha urais, tutakuwa kiungo muhimu kinachofanya kazi kwa uaminifu na nchi wanachama na taasisi zote," alisema Boka.

Yapi yanayotia wasiwasi pale Hungary itakapochukua hatamu za uongozi? 

Profesa wa sheria za Ulaya katika chuo kimoja cha HEC mjini Paris Alberto Alemanno, amekuwa akipigia upatu Hungary kutopewa urais wa Umoja wa Ulaya.

Hungary imekuwa ikipinga mipango mingi ya Umoja wa Ulaya tangu kuisaidia Ukraine katika vita dhidi ya Urusi hadi sera za uhamiaji za umoja huo.Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Anasema kwamba wasiwasi wake mkubwa kuhusu urais wa Hungary ni kwamba utahalalisha wazo la kwamba nchi mwanachama mwasi inaweza kukiuka sheria za mchezo na bado ikanufaika," aliiambia DW katika taarifa yake.

Alemano pia anaamini kuwa urais wa Hungary unaweza kuathiri sera muhimu za mazingira za Umoja wa Ulaya, na hasa kuyafikia malengo ya mwaka 2030 ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Eneo moja ambapo kunaweza kuwa na athari ni hatua ya awali ya Ukraine ya kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Kyiv inatarajia kuendeleza mazungumzo juu ya mageuzi muhimu.