Uregezaji wa masharti ya biashara uko kwenye misingi dhaifu nchini Libya
7 Novemba 2008Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi amesema nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ya Afrika Kaskazini mwanachama wa Shirika la Nchi Zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC haina chaguo bali kujirekebisha kwa kuendana na uchumi wa dunia ili kuweza kulinda faida za mfumo wa kijamaa wa Kiislam ambao ameuanzisha nchini humo baada ya kunyakuwa madaraka hapo mwaka 1969.
Vikwazo kwa mtaji wa kibinafsi vimeregezwa na Walibya kwenye nyadhifa za raha za serikali wanashajishwa kupata upya mafunzo na kuanzisha biashara kwa msada wa mikopo nafuu.
Lakini wachambuzi wa ndani ya nchi wanasema baadhi ya vigogo wa mapinduzi,jeshi na wa makabila ambao baadhi yao wanafaidika na ukiritimba wa taifa wanapinga mabadiliko katika elimu,afya na huduma.
Sami Zaptia wa kampuni ya kutowa huduma ya Ijue Libya yenye makao yake mjini Tripoli amesema bado kuna wajamaa vichwa mchungu ndani ya mfumo wenyewe na wengine wenye kutanguliza mbele maslahi yao.
Ameongeza kusema kwamba inabidi wasubiri kipindi cha kizazi kizima kabla ya kusonga mbele na mageuzi halisi ya kiuchumi.
Ziara katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli unaopakana na bahari ya Mediterranean inaonyesha mabadiliko fulani.
Anga ya mji huo imebadilika kutokana na kuchipuka kwa mahoteli mapya kuhudumia mmiminiko wa wafanyabiashara wa kigeni wanaovutiwa na ahadi ya kondarasi za kuvutia kuboresha miundo mbinu iliochakaa.
Serikali inasema inakusudia kuwaandikisha wafanyakazi wa kigeni milioni 1 wakiwemo Wabangladesh na Wasrilanka katika kipindi cha miaka mitano ijayo kujenga nyumba, vyuo vikuu na barabara.
Mtetezi mkuu wa mabadiliko hayo nchini Libya ni mtoto wa kiume wa Gaddafi Saif al- Islam ambaye hashikilii wadhifa wowote ule wa serikali lakini amethibitisha ushawishi wake kwa kuwa na dhima muhimu katika mazungumzo ya usuluhishi kuitowa nchi hiyo kwenye kutengwa kidiplomasia.
Mtoto huyo wa Gaddafi akilalamika juu ya wizara zisizokuwa na ufanisi na maafisa wa serikali wanaopokea rushwa amesema hapo mwezi wa Machi serikali inapaswa kuwapa wananchi moja kwa moja utajiri wake wa mafuta ili kwamba waweze kuchaguwa wapi pa kupata huduma za msingi.
Wataalamu wanasema serikali yumkini ikaepuka kutowa fedha taslimu na badala yake kuzipitishia fedha hizo kwenye mfuko wa kiuchumi na maendeleo ambao utawapa wale walio maskini kabisa Walibya milioni moja fungu katika mali zenye kuzalisha utajiri.
Mchambuzi wa kisiasa na profesa wa chuo kikuu Mustafa Fetouri amesema ukweli kwamba hakuna wito rasmi wa mageuzi hicho ni kikwazo.
Wanataaluma na wachumi waliozaliwa Libya ambao wameshajiishwa kurudi nyumbani kutoka nje kusaidia kujenga mustakbali wa nchi yao inaonekana wameemewa na kazi hiyo pevu.
Bodi ya Maendeleo ya Kiuchumi ilikuwa na lengo la kuwapatia mafunzo mamia ya wafanya biashara lakini inaelezwa kwamba majaribio yake ya awali kwa kiasi kikubwa yameshindwa.
Jambo hilo linawafanya baadhi ya watu wajiulize nani atafanya kazi katika maeneo ya teknolojia na biashara yanayotarajiwa kujengwa kwa takriban na wafanyakazi wa kigeni.
Miradi iliotangazwa katika miaka ya hivi karibuni inadokeza kwamba Libya inataka kuiga mafanikio ya Dubai, Qatar na Abu Dhabi ambazo zimeutanuwa uchumi wao wenye kutegemea mafuta kwa kuvutia wataalamu wa kigeni kujenga kanda huru za biashara,huduma za biashara na viwanda vipya.
Lakini wachambuzi wa kigeni wanasema Libya inahitaji kwanza kuzifanyia mageuzi taasisi zake za taifa.