1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno ina hakika kucheza fainali za Euro 2020

Sekione Kitojo
18 Novemba 2019

Mabingwa watetezi kombe la mataifa ya Ulaya Ureno yajihakikishia nafasi aktika fainali za Euro 2020, England nayo yafuata nyayo baada  ya kuishinda  Kosovo. Ujerumani yaongoza katika kundi C ikiwa pamoja na Uholanzi,

UEFA EURO 2020 - Portugal - Ukraine
Picha: picture-alliance/D. Shamkin

Mabingwa watetezi wa  kombe  la  mataifa  ya  Ulaya  Ureno imejihakikishia nafasi katika  kombe  la  Euro 2020  kwa  kuichapa Luxembourg , wakati England  imemaliza  kampeni  yake  ya  kufuzu kwa  ajili  ya  michuano hiyo kwa  ushindi  wa  mabao 4-0 dhidi  ya Kosovo jaan  Jumapili.

Wachezaji wa Uingereza Jadon Sancho na Harry Kane wakipongezana baada ya kupata bao dhidi ya KosovoPicha: picture-alliance/empics/A. Davy

Mabingwa wa  dunia  Ufaransa waliishinda  Albania  kwa  mabao 2-0 mjini  Tirana  na  kumaliza kileleni  mwa  kundi H,wakiwa  na  pointi 25, pointi mbili mbele  ya  Uturuki , ambao nao  walipata  ushindi wa mabao 2-0 dhidi  ya  Andora.

Siku mbili za  mwisho za michuano ya kufuzu  kuingia  katika  fainali  za  Euro 2020 zinaendelea  leo Jumatatu kwa  michezo kati ya  Gibraltar dhidi  ya  Uswisi, Ireland inaikaribisha  Denmark, katika  kundi D, wakati Malta  itakuwa mwenyeji  wa  Norway, Uhispania ikipimana  nguvu  na  Romania katika  kundi F na kundi J Ugiriki ina  miadi  na  Finland, Italia itakamilisha  ratiba  tu dhidi  ya  Armenia na Liechtenstein inapambana  na  Bosnia  Herzegovina.

Mshambuliaji  wa Ureno  na  klabu ya Juventus Turin ya  Italia, Cristiano Ronaldo amepachika  wavuni  bao  lake  la  99  katika  mchezo  wa kimataifa  wakati  akiiongoza  tena  Ureno  mabingwa  watetezi  wa kombe  la  mataifa ya  Ulaya  kupata  nafasi  katika  fainali  za  Euro 2020 dhidi  ya  Luxembourg.

Mshambuliaji  wa  Iran Ali Daei anashikilia  rekodi  ya  dunia  akiwa na  mabao  109 katika  michezo  ya  kimataifa mabao  aliyofunga katika  michezo 149  aliyoshiriki  kati  ya  mwaka  1993  na 2006.

Kikosi cha timu ya taifa ya UholanziPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Uholanzi yarejea katika  nafasi yake

Mlinzi  Virgil van Dijk  amesema  Uholanzi , imerejea  pale inapostahili, baada  ya  kukamilisha  kufuzu  kucheza  katika  fainali za  ubingwa  wa  mataifa  ya  Ulaya  Euro 2020.

Uholanzi ambayo  haikufuzu  kucheza  katika  Euro 2016 ama  kombe la  dunia  mwaka  2018  nchini Urusi, imefanikiwa  kusonga  mbele katika  fainali  hizo mwakani  ikiwa  bado  mchezo  mmoja baada  ya sare  tasa  hapo  jana  dhidi  ya  Ireland ya  kaskazini.

Wakati  fainali  hizo  zitafanyika  katika  viwanja  12  barani  Ulaya , Uholanzi  inaweza  kucheza  michezo  yake  ya   awamu  ya  makundi katika  uwanja  wa  Johan Cruyff Arena  mjini  Amsterdam , ambapo upangaji  wa  makundi  utafanyika  Novemba  30.

Mshambuliaji wa Ujerumani Serge GnabryPicha: AFP/P. Faith

Kikosi cha  kocha  Ronald Koeman  kinashikilia  nafasi  ya  pili katika  kundi  C, pointi  mbili  nyuma  ya  viongozi Ujerumani , timu pekee  iliyowashinda  katika  michuano  hiyo ya  mchujo.

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew amekisifu kikosi chake anachokijenga  upya  kwa  ajili ya  fainali za  Euro 2020 na  ametoa wito wa  ushindi dhidi ya  ireland ya  kaskazini kesho Jumanne na kujihakikishia  kufuzu kutoka  kundi F.

Mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo , CR7 (kulia) akipambana na mchezaji wa Ukraine Yevhen KonoplyankaPicha: picture-alliance/AP/E. Lukatsky

Ujerumani iliishinda  Belarus  kwa  mabao 4-0 siku  ya  Jumamosi ,wakati Uholanzi itakuwa  ikitimiza  wajibu  dhidi  ya  Estonia  ambayo haijapata ushindi  katika  kundi  hilo kesho Jumanne.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW