Ursula von der Leyen aahidi kusaidia usalama wa Sahel
2 Agosti 2017
Waziri Ursula von der Leyen amesema Ujerumani na Ufaransa zinataka kwa pamoja kupeleka wanajeshi 5000 katika nchi za Ukanda wa Sahel, katika juhudi za kuzuia kuenea kwa makundi yenye itikadi kali za kiislamu. Katika baadhi ya nchi alizozizuru, waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani alikuwa pamoja na mwenzake wa Ufaransa, Florence Parly.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bamako baada ya mazungumzo na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo, von der Leyen amesema mkutano wao umejikita juu ya kupelekwa kwa kikosi kitakachojulikana kama G5 Sahel, ambacho kitajumuisha maafisa kutoka nchi tano za ukanda huo, ambazo ni Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.
Nchi hizo zilifikia makubaliano mwaka 2014 ya kuunda kikosi cha pamoja cha kupambana na makundi ya itikadi kali, zikisaidiwa na Ujerumani pamoja na Ufaransa. Hata hivyo, alisema von der Leyen, lengo kubwa ni hatimaye kuuwezesha ukanda huo wa Sahel kujitosheleza wenyewe katika mahitaji ya ulinzi.
''Lengo muhimu kwetu, ambalo pia ni endelevu, ni kuona kwamba kanda hii inaweza kusimamia usalama wake yenyewe.'' Amesema von der Leyen, ambaye ameongeza kuwa msaada kwa eneo hilo utakuwa lengo kuu la hatua za pamoja za Ufaransa na Ujerumani mwezi ujao wa Septemba.''
Mkutano mjini Berlin
Hatua hizo za mwezi Septemba anazozizungumzia waziri von der Leyen, ni mkutano wa mjini Berlin utakaoitishwa kwa ushirikiano baina ya Ufaransa na Ujerumani, kujaribu kuziingiza nchi nyingine katika mchakato huo wa usalama katika ukanda wa Sahel. Tayari Uhispania na Italia zimekwishaelezea utashi wa kujiunga na mpango huo. Umoja wa Mataifa utashiriki katika mkutano huo, hali kadhalika Umoja wa Ulaya ambao tayari umekwishaahidi kuupiga jeki mpango huo kwa kiasi cha dola milioni 59.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly aliyekuwa na von der Leyen nchini Mali, alisema ziara yake ni mwendelezo wa juhudi za Rais Emmanuel Macron nchini Mali mwezi uliopita, ambamo rais huyo mpya wa Ufaransa alijitolea kuunga mkono vita dhidi ya makundi ya jihadi.
Ufaransa kuchangisha fedha za msaada
Waziri Parly alisema Ufaransa inajaribu kusaidia kuchangisha kiasi cha dola milioni 480 zitakazohitajika kuendeshea operesheni za kikosi cha G5 Sahel, ikizingatiwa kuwa nchi tano zinazounda kikosi hicho ni miongoni mwa mataifa masikini kabisa duniani. Inaarifiwa kuwa Rais Macron ameweza kupata uungaji mkono wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, kwa kiwango ambacho hakijawekwa bayana.
Ziara ya waziri Ursula von der Leyen Magharibi mwa Afrika ilianzia Gao, Kaskazini mwa Mali, ambako marubani wawili wa ndege ya kijeshi ya Ujerumani walikufa katika ajali ya helikopta. Waziri huyo alishiriki katika ibada ya kuwakumbuka marubani hao, na kuzungumza na wanajeshi wenzao.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre, dw
Mhariri: Iddi Ssessanga