1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Von der Leyen kuongoza tena Halmashauri ya Ulaya

18 Julai 2024

Bunge la Ulaya limemchagua Ursula von der Leyen kuwa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya kwa awamu ya pili, kwa kura 401. Von der Leyen alihitaji angalau kura 361 kati ya viti 720 ili kurejea kwenye kiti hicho.

Strassbourg 2024 | Von der Leyen | Uchaguzi wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akishangilia baada ya kuchaguliwa kuongoza kwa awamu ya pili, Julai 18, 2024Picha: Johanna Geron/REUTERS

Mwanamke huyo wa kwanza kuiongoza Halmashauri Kuu ya Ulaya aliipigania nafasi hiyo kwa kutetea rekodi yake ya awali ya kukabiliana na changamoto akiangazia hasa namna alivyoongoza juhudi za kulidhibiti janga la UVIKO-19, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji na uhaba wa makazi.

Soma pia:Uchaguzi wa bunge la Ulaya waanza Uholanzi

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2019, von der Leyen alishinda kwa tofauti ya kura tisa tu, tofauti na mwaka huu ambapo ameongoza kwa kura 40. Amepingwa kwa kura 284, na wabunge 15 hawakupiga kura. Kura saba ziliharibika.

Soma pia: Viongozi wa EU wamteua rasmi Ursula von der Leyen kuwa mkuu wa Tume ya Ulaya

Kwenye hotuba yake mbele ya Bunge la Ulaya baada ya kuchaguliwa, von der Leyen ameahidi kuchukua hatua kuimarisha uchumi wa Ulaya na katika sekta ya ulinzi. Ameahidi pia kuilinda demokrasia.

Aliwaambia wabunge hao kwamba alikuwa "tayari kuongoza vita" dhidi ya makundi ya kisiasa ya itikadi kali.

Bunge la Ulaya ambalo kwa sasa lina makundi mawili mapya ya mrengo wa kulia, limekutana mji wa Strasbourg nchini Ufaransa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa uchaguzi wa Ulaya ambao umeshuhudia kuongezeka kwa uungwaji mkono wa siasa za mrengo wa kulia.

Soma pia:Von der Leyen atetea kushirikiana na vyama vya mrengo wa kulia bungeni

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen(kushoto) na Spika wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola katika picha ya pamoja katika uchaguzi wa Umoja wa Ulaya, 2024.Picha: Johanna Geron/REUTERS

Von der Leyen aidha alitangaza ufadhili mpya wa Umoja wa Ulaya wa kuimarisha ushindani wa uchumi na maendeleo ya viwanda kwa kutumia teknolojia ya nishati safi na kuahidi kushughulikia suala la makaazi katika Umoja wa Ulaya, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa sera hiyo kuongezwa kwenye majukumu ya Halmashauri hiyo ya Ulaya.

Von der Leyen aahidi kupunguza uzalishaji wa kaboni

Hatua nyingine ni kuweka lengo kisheria la kupunguza uzalishaji wa kaboni ndani ya Umoja wa Ulaya kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2040.

Von der Leyen pia amependekeza kuimarisha udhibiti wa mipaka ya Umoja wa Ulaya na kuongeza mara tatu idadi ya walinzi wa mipakani na wa pwani hadi 30,000, huku akiainisha mipango wa kuiimarisha polisi ya Ulaya ama Europol, inayosimamia sheria ya Ulaya.

Soma pia: Mwaziri wa Uhamiaji wakutana Brussels kujadili mustakabali wa waomba hifadhi

Waziri huyo wa zamani wa Ujerumani, pia ameahidi kuanzisha tume mpya ya ulinzi itakayosaidia kujenga "Muungano wa dhati wa Ulinzi wa Ulaya" kwa ajili ya sekta ya silaha. Kwenye sera iliyochapishwa kabla ya kura hii, von der Leyen alisisitiza kwamba mataifa ya Ulaya yatawajibika wakati wote kwa ajili ya majeshi yao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW