1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uruguay imeingia Robo-finali kwa kuitoa Korea ya Kusini 2:1

26 Juni 2010

Na vipi Ghana dhidi ya Marekani leo usiku ?

Uruguay yaitoa Korea Kusini 2:1Picha: AP

Mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia-Uruguay , wameitoa Korea ya Kusini nje ya robo-finali kwa mabao 2:1.Hadi dakika ya 79 ya mchezo, timu hizo mbili zilikuwa suluhu bao 1:1 na zikijiandaa kurefusha mchezo. Lakini,Luis Suarez, alietia bao la kwanza,alirudi kutia bao la pili lililokua kitanzi kwa wakorea ya kusini. Suarez,alitangulia kutia bao lao la kwanza katika lango la mnamo dakika ya 8 ya mchezo.Alikuwa Diego Forlan, alietayarisha bao hilo. Korea ya kusini ilicheza na Cha,ambae tangu yeye hata baba yake wameicheza Frankfurt katika Bundesliga. Wakorea, walijitahidi sana kipindi cha kwanza na hasa Cha kusawazisha bila mafanikio. Mnamo dakika ya 75 wakorea wakasawazisha,lakini punde si punde,Suarez akalifuta bao lao mnamo dakika ya 80 ya mchezo .

Katika duru hii ya kutoana ,anaeshindwa anatoka moja kwa moja.Uruguay, ambayo iliitoa Mexico kwa bao 1:0 ili kupanga miadi na Korea ya Kusini, inatamba tena na mshambulizi wao hatari, Diego Forlan, aliekwishatia mabao 2 hadi sasa.Uruguay, haiktiwa bao katika duru ya kwanza na hii ni ushahidi wa ngome yao imara.Iwapo akina ,Cha,Lee,cho, wataweza kuvunja tumbu ya lango la wauru,tusubiri kuona dakika zinazokuja. Wauru,mabingwa mara 2 wa dunia, wanadai huu ni mwaka wao.kwani,tangu walipoilaza Brazil, nyumbani Rio de Jeneiro, 1950,na kuvaa taji lao la pili la dunia, wauru hawahesabiwi tena miongoni mwa miamba ya dimba duniani.Wanataka kubadili hali hiyo mwaka huu.

Endapo Uruguay,mwishoe, itaondoka na tikiti ya robo-finali leo, rais wao Jose Mujica, ameahidi kufunga safari ya Afrika kusini kwa Kombe hili la dunia ambayo hajaipanga kabla.

Timu 4 zinazoanza duru hii ya pili ya kutoana ya Kombe la dunia hii leo-mabingwa wa kwanza wa dunia Uruguay,Korea ya Kusini,Marekani na Ghana, hazikudhaniwa kabisa kuwa zina uwezo wa kuwasili hadi nusu-finali ya Kombe hili ambalo tayari, limewavua taji mabingwa Itali na kuwarejesha nyumbani makamo-bingwa Ufaransa. Leo lakini Uruguay iko uwanjani wakati huu na Korea ya Kusini na leo usiku ni zamu ya Black Stars-Ghana ikiwania tiketi hiyo ya nusu-finali ikiitoa Marekani. Timu hizi 4 -mojawapo yaweza kuwasili nusu-finali mara hii.

Marekani, ilinyakua tiketi yake kwa mpambano wa leo usiku kwa bao lao la dakika za kufidia katika lango la Algeria.

Ghana , kwa mara nyengine tena baada ya 2006 hapa Ujerumani, inawakilisha tena Afrika katika duru ya pili ya Kombe la Dunia, baada ya kuitoa jasho Ujerumani na kumaliza nafasi ya pili katika kundi lao D,licha ya kuzabwa bao 1:0.

Korea ya Kusini, ilio uwanjani wakati huu na Uruguay,ilitoka sare 2:2 na Nigeria na baadae ikahakikisha inaifuata Argentina duru hii ya pili .

Uruguay ilizabwa bao 1:0 na Mexico ,lakini ilitosha kupanga miadi duru hii ya pili na Argentina.

Kati ya timu hizi 4 zinazoanza duru hii ya pili leo, ni Ghana tu ambayo haikuwahi kufika nusu-finali ya Kombe la Dunia: Uruguay, imetawazwa mabingwa wa dunia mara 2:nyumbani 1930 na tena Brazil, 1950.

Marekani ,ilifika nusu-finali lilipoanzishwa Kombe hili 1930 na kupigwa kumbo na Argentina hatua hiyo.

Korea ya Kusini, ikiongozwa na kocha mdachi,Guus Hiddink, ilitamba hadi nusu-finali ilipoandaa kombe hili nyumbani 2002 na kuzimwa na Ujerumani .

Ujerumani nayo ilipokonywa Kombe na Brazil ilipotamba na Ronaldo.

Ghana, ilitamba 2006 hapa Ujerumani, ilipokuwa timu pekee ya Afrika kucheza duru ya pili kama mara hii,lakini, ikapigwa kumbo na Brazil.

Timu ya pili ya Afrika iliopigiwa upatu nayo ingetamba kama Ghana, ilikua Ivory Coast. Lakini,Tembo, walikuwa na kibarua kigumu jana kuizaba Korea ya Kaskazini zaidi ya mabao 8 ili kufuta yale 7 ya Ureno na kutumai Brazil ,

inailaza Ureno.Brazil na Ureno, zikatoka suluhu 0:0 wakati Korea ya Kaskazini haikuwaachia Tembo wa Corte d'Iviore, kumimina wavuni mwao zaidi ya mabao 3.

Ivory Coast,kama Bafana Bafana, Kameroun,Nigeria na Algeria ,zimefungishwa virago kurudi nyumbani.

Kocha wa Ivory Coast, Eriksson,zamani kocha wa Uingereza, aliueleza mpambano wa jana hivi:

"Nadhani timu hii imekuwa ikicheza uzuri.Ilikuwa taabu sana kushinda leo kwa mabao 7 au 8 ili kuweza kuingia duru ijayo."

Alisema kocha Eriksson,ambae kama kocha wa Bafana Bafana,Carlos Parreira na kocha wa Kameroun,Paul Le Guen,wanaachana na timu zao baada ya Kombe hili la Dunia.

Sasa matumaini ya bara zima la Afrika, yanawekwa kwa "nyota nyeusi-Black Stars"-Ghana leo usiku kuipiga tena kumbo Marekani kama ilivyofanya 2006 hapa Ujerumani na kukata tiketi ya robo-fainali.

Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia 2010 bila kujali matokeo ya leo usiku,imeshaipongeza Ghana kwa kukata tiketi ya duru hii ya pili,ikiwa ni timu pekee ya Afrika. Waghana wameingia duru hii licha ya kulazwa bao 1:0 na Ujerumani,bao maridadi ajabu alilotia mjerumani wa asili ya kituruki:Mesut Özil.

Akikumbusha jinsi alivyotia bao hilo,Özil alisema,

"Mbele yangu hakujakuwapo yeyote.Nikauchapa mkwaju mkali na mpira ukaingia ndani.Bila ya shaka, ni mwenye furaha kubwa."

Alisema, Özil, baada ya bao lake lililoweka miadi kesho Jumapili na Uingereza (England).Mpambano wa kesho, ni wa kukata na shoka ,una jazba na kama wa kulipiziana kisasi cha fainali ya 1966 pale bao la kutatanisha la Uingereza,liliinyima Ujerumani taji.

Taarifa kutoka Johannesberg, zinasema kwa mpambano huu wa kesho ,usalama unaimarishwa mjini Bloemfontein.

"Kuna uhasama kidogo kati ya timu hizi mbili siku za nyuma na bila shaka tutazingatia hayo kuimarisha usalama."

Msemaji wa kikosi cha Polisi cha Afrika Kusini aliarifu. Mashabiki wa timu hizi 2 kali za Ulaya wanajulikana kupeana changamoto na magazeti ya kila upande yameanza kucheza dimba lao.

Mara ya mwisho Ujerumani na Uingereza , zilipokutana miaka 10 iliopita, ilikua katika kinyan'ganyiro cha Kombe la Ulaya nchini Ubelgiji.Mitaa ya Charleroi,iligeuka medani ya vita kana kwamba, vita vya pili vya dunia,havikumalizika, 1945.

Zaidi ya mashabiki 500 wa pande zote mbili walitiwa nguvuni huko Ubelgiji.Ndege za kijeshi zilitumiwa kuwasafirisha mashabiki-wahuni waliotiwa pingu.Afrika Kusini , imeazimia kutoruhusu mkasa kama huo kurudiwa hapo kesho.

Upande wa vinywaji vya pombe ,waandazi wa Kombe la Dunia, tayari wamehakikisha vilabu vya pombe mjini Bloemfontein, vimesheheni vinywaji vikali ili kukidhi mahitaji ya maelfu ya mashabiki . Pengine, hiyo haikuwa busara njema. Kiasi cha mashabiki 25,000 wa Uingereza , wanatazamiwa kutia fora Bloemfontein.kikosi cha mashabiki wa Ujerumani kinakisiwa kuwa 10.000.

Uingereza, iliitoa Slovenia kwa bao 1:0 Jumatano wakati Ujerumani,iliilaza Ghana.

Uwanja ni wazi kwa marudio ya finali ya Kombe la Dunia, 1966.Tutumai mara hii, timu bora itashinda .

Je, Ghana,itafika robo-finali na baadae nusu-finali ? Tusubiri tuone leo usiku.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE

Uhariri:Mohamed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW