1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi baada ya kitisho cha uasi

Angela Mdungu
25 Juni 2023

Mamluki wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Wagner wameanza leo kurejea kwenye kambi zao baada ya kiongozi wao Yevgeny Prigozhin kukubali kwenda uhamishoni nchini Belarus.

Russland | TV Ansprache Putin
Picha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin/REUTERS

Hatua hiyo inafuatia hatua ya Rais Vladmir Putin kuafiki makubaliano ya kutoa msamaha. Makubaliano hayo yanaonekana kukomesha mara moja tishio la Yevgeny kuwa jeshi lake lingeweza kuuvamima mji wa Moscow. Hata hivyo wachambuzi wanasema kuwa uasi wa Wagnerumeonesha udhaifu katika utawala wa Putin.

Pamoja kitisho hicho kukoma, hatua za kiusalama za kupambana na ugaidi ziliendelea kuzingatiwa Moscow Jumapili. Kwa sasa, Prighozhin hajulikani aliko. Wanajeshi wake tayari wamekwishaondoka katika makao makuu ya jeshi ambayo waliyadhibiti kusini mwa Urusi.

Gavana wa Voronezh ambako misafara ya wanajeshi hao ilikuwa ikipita kuelekea Moscow amesema kuwa vikosi vya Wagner vilikuwa vikiondoka na sasa vikwazo vilivyokuwa vimewekwa vimeondolewa.

Mamlaka za mkoa wa Lipetsk kusini mwa Urusi nazo zimesema pia kuwa vikosi vya Wagner vilivyokuwa kwenye eneo hilo tangu Jumamosi sasa vimeondoka kwenye eneo hilo baada ya makubaliano yaliyosasababisha kusitishwa kwa uasi.

Mvutano wa muda mrefu

Mvutano wa muda mrefu kati ya Prigozhin na uongozi wa juu wa jeshi ulizidi kushika kasi Jumamosi baada ya kiongozi huyo wa Wagner kutangaza kuwa wanajeshi wake wanaidhibiti kambi ya jeshi mjini Rostov-on Don.

Putin alitoa hotuba ya dharura kwa njia ya televisheni akitaja hatua hiyo ya Wagner kuwa ni uhaini na aliapa kuwa waliohusika wataadhibiwa.

Kiongozi wa Wagner; Yevgeny PrigozhinPicha: Prigozhin Press Service/AP Photo/picture alliance

Saa kadhaa baada ya tangazo la kushtukiza la Prigozhin kuwa wapiganaji wake hawatasonga mbele ili kuepuka umwagaji damu, Ikulu ya Kremlin ilitangaza kuwa mshirika huyo wa zamani wa Putin angeondoka kuelekea Belarus nakuwa yeye na wanajeshi wa Wagner hawatoshtakiwa.

Licha ya kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko kusema kuwa alifanya majadiliano ya kumshawishi Prigozhin kuweka silaha chini, waangalizi wanasema hatua ya kiongozi huyo anayeonekana kuwa mshirika mdogo wa Putin kuingilia kati mzozo huo ni aibu.

Uwezekano wa kitisho kingine cha usalama 

Naye Jenerali wa zamani wa jeshi la Uingereza,Richard Dannatt akizungumzia yanayoendelea Urusi ametahadharisha kuwa huenda mamluki wa Wagner wakafanya shambulio kutokea Belarus ikiwa idadi kubwa ya wapiganaji hao watamfuata kiongozi wao. Kufikia sasa haijafahamika ikiwa watamfuata Prigozhin nchini Belarus.

Mamluki wa Wagner walipokuwa mjini RostovPicha: Erik Romanenko/TASS/dpa/picture alliance

Wakati hayo yakiendelea  mataifa kadhaa yamejitokeza kuiunga mkono Urusi katika kukabiliana na uasi uliojitokeza. Balozi wa Urusi nchini Korea Kaskazini Alexander Matsegora amekutana na Naibu waziri wa mambo ya kigeni Im Chon II na kusema kuwa anaamini uasi wa kijeshi uliojitokeza Urusi utadhibitiwa kwa mafanikio makubwa.

Awali, ofisi ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ilitoa taarifa yake Jumamosi, ikisema kuwa iko tayari kusaidia mzozo wa ndani kati ya Urusi na kundi la Wagner. Ofisi hiyo  kupitia mtandao wa tweeter iliandika Ankara inaweza kusaidia kutatua mzozo haraka iwezekanavyo.

Katika hatua nyingine, wizara ya mambo ya kigeni ya China imeripoti kupitia tovuti yake kuwa, naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Andreui Rudenko ameelekea China kufanya mazungumzo juu ya "masuala ya kimataifa" yakiwemo masuala ya kikanda yanayozihusu nchi zote mbili. Haikuwekwa wazi ikiwa ziara ya Rudenko inatokana na uasi uliofanywa na mamluki wa Wagner hivi karibuni au la.

Itakumbukwa kuwa, kundi la mamluki la Wagner limekuwa likihusishwa kufanya operesheni zake katika baadhi ya mataifa ya Afrika yakiwemo Mali na Sudan.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW