1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Daraja muhimu la Krimea laharibiwa na mlipuko wa lori

8 Oktoba 2022

Urusi imetangaza kuwa daraja linaloiunganisha na rasi iliyochukua ya Krimea limeharibiwa kufuatia mlipuko wa lori uliosababisha moto mkubwa. Imeapa kuwakamata washukiwa, lakini bila ya moja kwa moja kuitaja Ukraine.

Krim | Brand auf der Brücke
Picha: REUTERS

Urusi imesema mlipuko huo wa bomu kwenye lori ulisababisha moto uliochoma mabehewa saba ya mafuta yaliyokuwa yakisafirishwa kwa treni na pia kusababisha sehemu za miundombinu hiyo inayojumuisha barabara na reli kuharibika.

Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 19 juu ya na kuunganisha bahari Nyeusi na bahari ya Azov lina vituo vya treni na vya magari.

Maoni ya wahariri juu ya Krimea

Picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha moto mkubwa kwenye daraja hilo na kusababisha sehemu zake kuporomoka hadi baharini.

Mashirika ya habari ya Urusi yamekinukuu kamati ya kitaifa ya kupambana na ugaidi ikithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa bomu lililokuwa kwenye gari lililipuka kwenye daraja hilo la Krimea Jumamosi asubuhi na kusababisha moto ulioteketeza mabahewa saba ya mafuta.

Moto katika sehemu ya daraja linalounganisha rasi ya krimea na Urusi. Kulingana na taarifa zilizothibitishwa na Urusi, moto huo ulisababishwa na bomu lililokuwa kwenye gari ambalo lililipuka na kusababisha moto kwenye mabehewa saba ya mafuta yaliyokuwa yakisafirishwa kwa treni.Picha: Alyona Popova/Tass/IMAGO

Daraja hilo lililozinduliwa rasmi na Rais Vladimir Putin Mwenyewe mwaka 2018, ni kiungo muhimu cha kupitisha zana za kivita, zinazopelekewa wanajeshi wa Urusi wanaopambana nchini Ukraine. Awali, Urusi ilishikilia kuwa daraja hilo ni salama licha ya vita vya Ukraine.

Spika wa jimbo la Crimea aituhumu Ukraine kuhusika na mlipuko huo

Spika wa bunge linaloungwa mkono na Urusi la jimbo hilo la Krimea aliituhumu Ukraine moja kwa moja kuhusika na mlipuko huo, lakini Urusi haikutoa tuhuma.

Mara kwa mara maafisa wa Ukraine wamekuwa wakitishia kushambulia daraja hilo. Punde tu baada ya mkasa ulioharibu daraja hilo, baadhi ya maafisa wa Ukraine walipongeza.

Juhudi za kuuzima moto kwenye daraja hilo kutumia helikopta baada ya mlipuko uliosababisha sehemu ya daraja hilo kuporomoka.Picha: Konstantin Mihalchevskiy/SNA/IMAGO

Afisa mkuu katika ikulu ya Ukraine Andrii Podolyak alichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter, picha iliyoonesha sehemu kubwa iliyoporomoka ya daraja hilo, kisha akaandika, "daraja la Krimea, huu ni mwanzo. Kila kitu ambacho ni kinyume cha sheria sharti kiharibiwe. Kila kitu kilichoibiwa sharti kirudishiwe Ukraine na kila kitu kinachokaliwa na Urusi kiondolewe".

Kumekuwa na milipuko kadhaa katika vituo vya kijeshi vya Urusi katika rasi ya Krimea. Ikiwa itathibitishwa kuwa Ukraine imehusika katika mlipuko wa hivi karibuni, basi itaashiria hali tofauti ikizingatiwa daraja hilo liko mbali na uwanja wa mapambano.

Japo Urusi iliikamata baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa rasi ya Krimea mwanzoni mwa uvamizi wake nchini Ukraine na kujenga njia kufikia Bahari ya Azov, Ukraine inaendeleza mashambulizi yanayolenga kuyakomboa maeneo hayo.

(Vyanzo: AFPE,APE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Hawa Bihoga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW