Marekani huenda ikaiwekea Urusi vikwazo ndani ya siku 50
17 Julai 2025
Rais wa Marekani Donald Trump amesema atatuma msaada wa kijeshi wenye thamani ya mabilioni ya dola kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na makombora ya ulinzi wa anga ya Patriot. Akizungumza Ikulu ya White House akiwa na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte, Trump alisema hatua hiyo inakuja baada ya kuvunjwa moyo na msimamo wa Rais Vladimir Putin, ambaye hadi sasa anakataa makubaliano ya amani.
Trump pia ametishia kuiwekea Urusi vikwazo vipya iwapo haitakubali mkataba wa amani ndani ya siku 50. Alisema vikwazo hivyo vitakuwa vya "asilimia 100" na vitawalenga pia mataifa yanayonunua bidhaa kutoka Urusi, ikiwa ni njia ya kuinyima mapato muhimu ya kigeni. Hii imechukuliwa kama hatua ya kuongeza presha ya kimataifa dhidi ya Moscow.
Kamanda wa NATO asema mifumo ya Patriot kupelekwa Ukraine
Kwa wachambuzi wengi, vikwazo hivyo vya sekondari vinaweza kuwa na athari kubwa zaidi kwa uchumi wa Urusi kuliko hatua zilizowahi kuchukuliwa awali, hasa ikizingatiwa kuwa nchi kama China na India zimekuwa soko kubwa la mafuta na bidhaa za Kirusi. Lakini mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, anaonya kuwa muda alioweka Trump ni mrefu mno kwa hali ya sasa ya kivita.
"Ni jambo zuri sana kwamba Rais Trump anachukua msimamo mkali dhidi ya Urusi. Hata hivyo, siku 50 ni muda mrefu sana tukizingatia kuwa watu wasio na hatia wanauawa kila siku. Ni wazi kwamba sote tunapaswa kuongeza shinikizo kwa Urusi ili nayo itake amani. Ni vizuri kuona Wamarekani wanachukua hatua, na ninatumaini pia wanatoa msaada wa kijeshi kama ambavyo Ulaya inafanya."
Licha ya vikwazo vingi dhidi ya Urusi bado uchumi wake unaendelea kukua
Licha ya vikwazo vingi, uchumi wa Urusi uliendelea kukua kwa kasi ya kushangaza—asilimia 4.1 mwaka 2023 na asilimia 4.3 mwaka 2024. Lakini ukuaji huo unaonekana sasa kufifia, huku wataalamu wakitabiri kushuka hadi asilimia 2, na Taasisi ya ifo ya mjini Munich ikitabiri kuporomoka kwa asilimia 0.8 mwaka 2026. Sababu kubwa ni viwango vya juu vya riba (asilimia 21) vinavyozuia uwekezaji.
Ruble imeimarika kwa karibu asilimia 40 dhidi ya dola tangu mwanzo wa mwaka, hali ambayo wachambuzi kama Vasily Astrov wa WIIW Vienna wanasema ilichochewa na matarajio ya mwelekeo wa urafiki kutoka kwa Trump. Lakini hali hiyo huenda ikabadilika endapo mswada mpya wa vikwazo unaoandaliwa na Seneta Lindsey Graham na kundi la maseneta wa vyama vyote utapitishwa kabla ya Agosti mosi.
Zeleskyy amshukuru Trump kwa ahadi ya msaada wa kijeshi
Mswada huo unalenga kuziwekea vikwazo nchi zote zinazonunua bidhaa za nishati kutoka Urusi—huku China na India zikiwa malengo makuu. Mwaka 2024, China ilichangia asilimia 40 ya uagizaji wa bidhaa Urusi na asilimia 30 ya uuzaji wake, ikisaidia pia sekta ya kijeshi kupitia njia kama Hong Kong. India pia ilikuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Urusi.
Ingawa vikwazo vya pili vilitekelezwa kwa ukali wakati wa utawala wa Biden, Trump alilegeza utekelezaji wake. Benki za Urusi kwa sasa zinatumia mfumo wa siri wa malipo unaoitwa Njia ya China, ili kuepuka vikwazo. Hata hivyo, Alexander Shokhin wa RSPP anaamini China haitatetemeka tena kwa vitisho vya vikwazo. Ikiwa hivyo, basi mashaka bado yapo kuhusu mafanikio ya shinikizo jipya la Trump kwa Urusi.