1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi imewafukuza Wanadiplomasia 23 wa Uingereza

Caro Robi
17 Machi 2018

Urusi imewafukuwa wanadiplomasia 23 wa Uingereza katika hatua ya kujibu uamuzi wa Uingereza kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi kufuatia kashfa ya kupewa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal nchini Uingereza.

UK | Nervengiftattentat auf Sergei Skripal - Ermittler in Schutzkleidung
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Matthews

Urusi ambayo inadaiwa kuhusika na kitendo hicho cha kupewa sumu kwa Skripal,  siku ya Jumamosi imetangaza kuwa inawapa muda wa wiki moja pekee wanadilpomasia 23 wa Uingereza kuondoka nchni humo na kusitisha shughuli za shirika la kimataifa la Uingereza la British Council nchini humo linalohusika na masuala ya elimu pamoja na ushirikiano wa kitamaduni.

 Hayo yanajiri baada ya  Urusi kumuita hii leo balozi wa Uingereza nchini humo Laurie Bristow ambapo pia wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imeonya kuwa serikali italazimika kuchukua hatua nyingine zaidi iwapo vitendo vingine visivyo rafiki vitafanyika dhidi yake.

Urusi yajibu hatua za Uingereza

Aidha Urusi pia imesitisha shughuli za ubalozi mdogo wa Uingereza ulioko katika mji wa St Petersburg. Alhamisi wiki hii, Uingereza ilitangaza inawafurusha wanadiplomasia 23 wa Urusi kutokana na kughadhabishwa na shambulizi la sumu dhidi ya Skripal mwenye umri wa miaka 66 na binti yake Yulia mwenye umri wa miaka 33 katika mji wa Salisbury. Wawili hao wako katika hali mahututi hospitalini.

Balozi wa Uingereza nchini Urusi Laurie BristowPicha: picture alliance/AP/A. Zemlianichenko

Urusi ambayo kesho Jumapili inafanya uchaguzi wa Rais unaotarajiwa kumpa ushindi  Rais Vladimir Putin imeonya kuwa iko tayari kuchukua hatua kali zaidi kujihami na kuilinda hadhi yao dhidi ya uhasama kutoka Uingereza na nchi nyingine za Magharibi.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema ilitarajia Urusi kuchukua hatua za kulipiza kisasi na kuongeza kuwa Baraza la kitaifa la Usalama litakutana mapema wiki ijayo kujadili hatua zaidi itakazochukua kuhusiana na shambulizi hilo la sumu nchini Uingereza.

Katika taarifa wizara hiyo ya mambo ya nje ya Uingereza imeongeza kusema wanachokipa kipaumbele hivi sasa ni kuwahudumia maafisa wake walioko Urusi na kuwasaidia wale waliorejeshwa nyumbani.

Urusi bado haijajieleza vya kutosha

Uingereza imesisitiza kuwa hatua ilizochukua Urusi haibadilishi ukweli kuwa jaribio la kuwaua watu wawili kwa kutumia sumu lilifanywa katika ardhi ya Uingereza na hakuna shaka Urusi ilihusika na jaribio hilo.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/Parliament TV

Urusi ambayo imekanusha kuhusika na shambulizi dhidi ya Skripal na binti yake imelalamika kuwa Uingereza imeshindwa kutoa ushahidi kuwa Urusi ndiyo ilihusika katika shamabulizi hilo la Salisbury na kuongeza kuwa imeshutushwa na wakati huo huo, kuchekeshwa na madai hayo yasiyo na msingi wowote na yasiyosameheka.

Siku ya Ijumaa, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson alisema kuna uwezekano mkubwa kuwa Rais Vladimir Putin ndiye alitoa maamuzi hayo ya kumshambulia Skripal kwa kutumia sumu inayoathiri neva.

Uingereza, Marekani, Ujerumani na Ufaransa kwa pamoja zimeitaka Urusi kutoa maelezo kuhusu shambulizi hilo lililotokea tarehe 4 mwezii Machi. Wachunguzi wa Urusi wamesema wameanzisha uchunguizi wa uhalifu kuhusu jaribio la kumuua Yulia Skripal na kuongezea wako tayari kushirikiana na maafisa wa Uingereza.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Isaac Gamba