1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi inaibua kitisho cha kiusalama Ulaya

6 Januari 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Ujerumani wamesema hatua ya Urusi ya kuongeza wanajeshi wake karibu na mpaka wa Ukraine inaibua kitisho cha ghafla na cha dharura dhidi ya usalama barani Ulaya.

USA Washington | Annalena Baerbock, Außenministerin & Antony Blinken, Außenminister
Picha: Mandel Ngan/REUTERS

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na Annalena Baerbock wa Ujerumani wamesema ni kwa maana hiyo uingiliaji wowote utasababisha hatua kali dhidi Urus. Baerbock amesema hayo katika ziara yake nchini Marekani. 

Hata hivyo hawakueleza wazi kuhusiana na hatua hizo, lakini pia namna wanavyoweza kufikia makubaliano katika masuala wanayotofautiana kuanzia kuiwezesha kijeshi Ukraine hadi mradi tata wa bomba la gesi la Nord Stream 2.

Blinken alisema "Ujerumani na Marekani zinaona hatua ya Urusi kuelekea Ukraine kama changamoto ya haraka na ya dharura kwa amani na utulivu barani Ulaya. Tunalaani hatua ya Urusi kujiimarisha kijeshi kwenye mipaka ya Ukraine, pamoja na matamshi makali ya Moscow."

Baerbock anaunga mkono matamshi ya Blinken kwa kusema kwa pamoja wanarejea kauli yao kuhusiana na shughuli zozote za Urusi ambazo wanaona zina madhara makubwa na iwapo itarudia kukiuka uhuru wa Ukraine, itarajie hatua kali kabisa dhidi yake.

Ametumia pia ziara hiyo kusisitizia kuhusu msimamo wa serikali yake juu ya mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2, akisema wamekubaliana kuidhibiti Urusi iwapo itautumia kama silaha.

Marekani na Ujerumani wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na mradi wa bomba la gesi unaotokea Urusi hadi Ujerumani.Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Baerbock alisema, "Tayari tumekubaliana kwamba pamoja na washirika wetu wa Ulaya tutachukua hatua madhubuti iwapo Urusi itatumia nishati kama silaha ama iwapo kutakuwa na hatua kali zaidi."

Soma Zaidi: Marekani na Ujerumani zafikia muafaka mradi wa bomba la gesi la Urusi

Hata hivyo Blinken hakutaka kuzungumzia hilo moja kwa moja na badala yake alisema tu kwamba Marekani itaendelea kushinikiza hatua za pamoja dhidi ya mradi huo na kushirikiana katika namna ambayo itakuwa sawa katika kushughulikia masuala ya nishati na changamoto zake.

Rais Joe Biden alianya mazungumzo ya simu ya marais wa urusi Vladimi Putin na Volodymir Zelensky kuhusiana na mzozo wa UkrainePicha: White House/imago images/ZUMA Wire

Mkutano kati ya Blinken na Baerbock unafanyika baada ya mazungumzo ya simu wiki iliyopita kati ya rais Joe Biden wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi, na kati ya Biden na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumapili, lakini pia majadiliano kati ya mshauri wa Biden wa masuala ya usalama wa taifa Jake Sullivan na wenzake kutoka mataifa matano ya kaskazini mwa Ulaya.

Lakini pia yanatangulia msururu wa mikutano itakayowakutanisha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, maafisa waandamizi wa Marekani na Urusi na shirika la masuala ya usalama na ushirikiano la Ulaya, iliyopangwa kufanyika wiki ijayo.

Hata hivyo Blinken tayari ameonyesha wasiwasi iwapo mikutano hii itazaa matunda, akisema suala kubwa ni iwapo Urusi inaamini katika diplomasia na kuondoa wanajeshi wake na kuongeza kuwa ni suala la kusubiri na na kuona matokeo ya mikutano hiyo.

Soma Zaidi: Biden na Putin kujadiliana matakwa ya Urusi kuhusu usalama

Baerbock ni waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Ujerumani katika serikali mpya kwenda Marekani katika kipindi cha miaka 16, nje ya utawala wa Angela Merkel, na ameonyesha msimamo mkali zaidi kueleka Urusi, tofauti na mtangulizi wake.

Mashirika: APE/DPAE

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi