1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi inasema bado haitolipiza kisasi

Oumilkheir Hamidou
30 Desemba 2016

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameondowa uwezekano wa kulipiza kisasi baada ya kufukuzwa wanadiplomasia wake 35 na Marekani kwa tuhuma za kuhusika na upelelezi na kwamba Urusi imeshawishi uchaguzi wa rais nchini Marekani.

China Treffen Putin Obama
Picha: picture-alliance/Sputnik/A. Druzhinin

Shirika la habari la RIA limemnukuu rais Vladimir Putin akisema atazingatia hatua zitakazochukuliwa na rais mteule Donald Trump atakaekabidhiwa hatamu za uongozi january 20 mwakani, kabla ya kupitisha hatua ziada kuhusu uhusiano kati ya Urusi na Marekani.

Hapo awali waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrow alimshauri rais Putin aamuru serikali ya mjini Moscow iwafukuze wanadiplomasia 35 wa Marekani na kuwazuwia wanadiplomasia hao wa Marekani kutumia majengo mawili yaliyoko mjini Moscow.

Hayo yamesababishwa na uamuzi wa rais Barack Obama wa kuwafukuza wanadiplomsia 35 wa Urusi wanaotuhumiwa kufanya upelelezi pamoja na kuyawekea vikwazo mashirika mawili ya upelelezi ya Urusi kwa tuhuma kwamba yamehusika katika udukuzi dhidi ya makundi ya kisiasa katika uchaguzi wa rais mwaka huu. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov amezitaja tuhuma kwamba Urusi imeingilia kati katika uchaguzi wa Marekani kuwa "hazina msingi."

Ubalozi wa Urusi mjini WashingtonPicha: picture-alliance/AP Images/J. Scott Applewhite

Hakuna yeyote atakaefukuzwa-anasema Vladimir Putin

Rais Vladimir Putin amelikataa pendekezo la waziri wake wa mambo ya nchi za nje:"Hatutomfukuza yeyote" amesema rais Putin katika taarifa yake. Ameongeza kusema pia kwamba anaviangalia vikwazo ziada kuwa sawa na hatua nyengine ya kuvuruga uhusiano kati ya Moscow na Washington. Amesema anasikitika kuona serikali ya Obama inamaliza mhula wake namna hiyo.

Maafisa wa Urusi wamevitaja vikwazo vya Marekani kuwa hatua ya mwisho ya rais aliyedhoofika na kuashiria uwezekano wa kumuona rais mteule Donald Trump akibadilisha mkondo wa mambo atakapokabidhiwa hatamu za uongozi january 20 inayokuja.

Hata hivyo wanachama kadhaa wa Republican hawavutiwi na fikra ya kuwepo usuhuba pamoja na Urusi na badala yake wanaunga mkono vikwazo dhidi ya Moscow. John McCain na Lindsey Graham, vigogo katika baraza la Senet, wameshasema watahakikisha vikwazo vikali zaidi vinawekwa dhidi ya Urusi.

Waziri mkuu wa zamani wa Urusi Dmitri MedvedevPicha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

 "Hatua za mwenye uchungu wa kukata roho" wanasema maafisa wa serikali ya Urusi

"Inasikitisha kwamba serikali ya Obama iliyoanza kwa kurejesha mshikamano kati ya nchi zetu,inamaliza mhula wake kwa "uchungu wa kukata roho." amesema Dmitry Medvedev aliyewahi kuwa waziri mkuu mnamo mwaka 2009 na kusaidia pale rais Barack Obama alipoanza juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Urusi.

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imekanusha ripoti za vyombo vya habari zinazodai kwamba maafisa wa serikali wameamuru shule ya kimarekani iliyoko mjini Moscow ifungwe.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW