1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Urusi inaweza kuipeleka silaha Korea Kaskazini?

27 Juni 2024

Makubaliano makubwa ya kiulinzi yaliyosainiwa hivi karibuni kati ya Korea Kaskazini na Urusi yanazidisha wasiwasi kwamba Urusi inaweza ikapaleka silaha Korea Kaskazini, na kubadilishana ujuzi na utawala wa Kim Jong Un.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Urusi, Vladmir Putin
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: VLADIMIR SMIRNOV/AFP/Getty Images

Kiongozi wa Korea Kaskazini alisaini makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati na Rais wa Urusi Vladmir Putin, wakati rais huyo alipoizuru Korea Kaskazini, wiki iliyopita. Makubaliano hayo yanahusisha kujizatiti na kujitolea kwa nchi hizo mbili kusaidiana pale mojawapo inaposhambuliwa.

Huku kukiwa hakuna kipengele kinachoonyesha kubadilishana silaha, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, umeifanya Moscow kuwa karibu na Pyongyang, huku mataifa ya Magharibi yakizidisha vikwazo dhidi ya Urusi. Inadaiwa kuwa Korea Kaskazini imetoa mamilioni ya mizinga na makombora ya masafa mafupi kwa wanajeshi wa Putin waliokuwa katika oparesheni nchini Ukraine.

Korea Kaskazini nayo imepokea mafuta ya Urusi kwa kiasi kinachozidi viwango vilivyoainishwa katika vikwazo vya Umoja wa Mataifa, akiba ya chakula na teknolojia kwa ajili ya mipango yake ya nyuklia, makombora na vyombo vya anga. Hata hivyo, Korea Kaskazini imekanusha madai ya kuipatia Urusi silaha.

Kombora lililorushwa na Korea KaskaziniPicha: KCNA/Reuters

Nico Lange, mtaalamu wa masuala ya usalama katika Mpango wa Ulinzi na Usalama kwenye kituo cha Uchambuzi wa Sera ya Ulaya, anasema Urusi inahitaji risasi za kivita na makombora kutoka Korea Kaskazini. Lange ameiambia DW kuwa Korea Kaskazini inaitumia fursa hiyo na kuna uwezekano mkubwa ikaomba kupatiwa ujuzi wa teknolojia ya makombora, mpango wake wa nyuklia na magari.

Utafiti wa mauzo ya nje ya Urusi uliofanywa na Kituo cha Stimson chenye makao yake mjini Washington na kuchapishwa kwenye tovuti yake ya North 38, unaonyesha kuwa Kim ana orodha ndefu ya manunuzi ya vifaa ambavyo angependa kupata ili kuvibadilisha na vile vya zamani.

Soma zaidi: Kim ausifu uhusiano unaotanuka wa Korea Kaskazini na Urusi

Ikiwanukuu maafisa wa Marekani, ripoti ya utafiti huo imeeleza kuwa Korea Kaskazini inajaribu kununua ndege za kivita, magari ya kivita na makombora ya kutoka ardhini hadi angani kutoka Urusi.

Katika ujumbe wake wa mtandao wa Telegram, Naibu Spika wa Bunge ka Urusi, Vyacheslav Nikonov alielezea mipango ya kutanua ushirikiano kati ya Urusi na Korea Kaskazini katika vyombo vya anga. Hilo huenda lilikuwa katika ahadi ya Putin kuisaidia Korea Kaskazini na mpango wa satelaiti, aliyoitoa wakati Kim alipokitembelea kituo cha vyombo vya anga cha Vostochny, mnamo mwezi Septemba.

Viongozi wa Korea Kaskazini na Urusi walipokitembelea kituo cha vyombo vya anga cha Vostochny, UrusiPicha: Sputnik/Mikhail Metzel/Kremlin via REUTERS

Yakov Zinberg, profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kokushikan, Tokyo, anasema kuwa Korea Kaskazini na Urusi zinatumia pamoja mpaka mfupi sana kaskazini mashariki mwa rasi na kuna daraja la reli juu ya Mto Tumen, ambalo tayari lilitumika kwa ajili ya treni zilizokuwa zimebeba makombora kuvuka hadi Urusi.

Kulingana na Zinberg, inajulikana kwamba meli zinasafiri kutoka bandari za Mashariki ya Mbali za Urusi hadi bandari ya Korea Kaskazini bila hata ya kuondoka kwenye eneo moja la maji la kila mmoja.

Meli za Korea Kaskazini zaonekana Urusi

Picha zilizopigwa na kampuni ya Marekani ya Planet Labs PBC na kuchapishwa na gazeti la Japan la Yomiuri Shinbun mnamo Juni 7, zinaonyesha kile kinachoaminika kuwa meli nne za Korea Kaskazini zilizotia nanga katika bandari ya Urusi ya Vostochny.

Zinberg ameiambia DW kuwa kimsingi Urusi na Korea Kaskazini zinapuuza vikwazo vilivyowekwa, na haziwezi kusema hilo kwa uwazi na zitaendelea kukanusha madai kwamba zinapeana silaha au mafuta, lakini zinaonyesha wazi kuwa hazijali kile jumuia ya kimataifa inakifikiria.

Zinberg anasema muungano huo wa kijeshi unazileta pamoja nguvu ya kijeshi ya Urusi na matarajio ya Kim katika ukanda huo, hivyo itabidi Korea Kusini, Japan na Marekani zichukue hatua za kukabiliana na makubaliano mapya ambayo yanaweza kuwa na nguvu sana.

(DW)