1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, Iran kusaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati

13 Januari 2025

Urusi na Iran zinatazamiwa kusaini makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu ya ushirikiano wa kimkakati Ijumaa hii, huku Umoja wa Ulaya ukitangaza msaada mpya kwa Ukraine.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran na Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Alexander Shcherbak/SNA/IMAGO

Taarifa iliyotolewa leo na Ikulu ya Kremlin imesema kwamba mnamo tarehe 17 Januari, Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Iran, Masoud Pezeshkian, watakuwa na mazungumzo maalum yatakayofuatiwa na utiaji saini wa kile kiitwacho mkataba wa ushirikiano wa kimkakati, ambao unajumuisha masuala kadhaa, yakiwemo ya ulinzi na usalama.

Viongozi hao wawili watajadiliana njia zaidi za kutanuwa na kuimarisha mafungamano baina ya Moscow na Tehran, ikiwemo biashara na uwekezaji, usafiri na masuala ya kibinaadamu, kwa mujibu wa Kremlin.

Soma zaidi:Urusi na Iran kutia saini mkataba mpya wa ushirikiano hivi karibuni

Wengi wanatazamia mkataba huo uliongojewa kwa muda mrefu unaweza kufanana sana na ule uliosainiwa hivi karibuni kati ya Urusi na Korea Kaskazini, ambao miongoni mwa vipengelea vyake ni ushirikiano wa kiulinzi ambao unaruhusu upande mmoja kuusaidia mwengine pale utakaposhambuliwa na nguvu kutoka nje.

Umoja wa Ulaya watuma msaada zaidi Ukraine

Hayo yanakuja wakati Kamisheni ya Ulaya ikitangaza hivi leo msaada mpya wa kibinaadamu wenye thamani ya euro milioni 142, kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya watu wa kusini na mashariki mwa Ukraine.

Kamishna wa Migogoro wa Umoja wa Ulaya, Hadja Lahbib.Picha: European Union

Fedha hizo zinakusudiwa kusaidia kwenye upatikanaji wa chakula, maji, huduma za afya na vifaa vya kuwalinda raia na baridi kali wakati huu wa msimu wa kipupwe barani Ulaya. 

Soma zaidi: Rais wa Iran ziarani China

Taarifa iliyotolewa na Kamisheni hiyo inakisia kuwa raia milioni 12.7 wa Ukraine wana uhitaji mkubwa wa msaada wa haraka.

Msaada huu mpya unafanya kiwango cha jumla cha misaada ya kibinaadamu iliyotengwa na Kamisheni ya Ulaya kwa Ukraine kufikia euro bilioni 1.1.

Tangazo hili limetolewa leo wakati Kamishna wa Migogoro wa Umoja wa Ulaya, Hadja Lahbib, akiitembelea Ukraine anakotazamiwa kukutana na Rais Volodymyr Zelensky.

Urusi yakosowa vikwazo vya Marekani, Uingereza

Katika hatua nyengine, Ikulu ya Urusi imekosowa vikali vikwazo vipya vya Marekani, ikiviita kuwa ni jaribio la kuyahujumu makampuni ya Kirusi kwa kanuni zinazoharibu ushindani.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov.Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amewaambia waandishi wa habari na hapa namnukuu: "Wakati huo huo, uamuzi kama huu unapelekea machafuko kwenye masoko ya kimataifa ya nishati na mafuta." Mwisho wa kumnukuu.

Soma zaidi: Marekani na Urusi zimetia saini mkataba wa START

Peskov ameongeza kwamba Moscow itafanya kila iwezalo kupunguza madhara ya vikwazo hivyo vilivyotangazwa juzi na Marekani na Uingereza, akisisitiza kuwa Urusi inao uwezo wa kuvihimili.

Kwa upande mwengine, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amekabidhi rasmi mizinga chapa RCH 155 kwa Ukraine kwa ajili ya kuimarisha uwezo ya nchi hiyo kushambulia.

Balozi wa Ukraine nchini Ujerumani, Oleksii Makeiev, aliipokea mizinga 54 mjini Berlin, ambapo sita kati yao itabakia Ujerumani kwa ajili ya kuwapa mafunzo wanajeshi wa Ukraine.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW