Urusi, Iran, Uturuki zawania kupata msimamo wa pamoja Syria
3 Aprili 2018Viongozi wa mataifa hayo matatu Vladimir Putin, Recep Tayyip Erdogan na Hassan Rouhani wa Iran watakutana mjini Ankara kwa mazungumzo yatakayohusu katiba mpya ya Syria na kuongeza usalama katika maeneo ambayo yametengwa bila ya shughuli za kijeshi nchini humo, wamesema maafisa wa Uturuki.
Mkutano huo wa kilele kuhusu Syria unawaleta pamoja mataifa mawili yenye nguvu ambayo yamekuwa waungaji mkono wakubwa wa rais Bashar al-Assad , Iran na Urusi , pamoja na mmoja kati ya wapinzani wake wakubwa Uturuki.
Ushirikiano baina ya kambi hizo zinazopingana unaongeza matumaini ya kuiimarisha Syria baada ya miaka saba ya mzozo ambamo watu 500,000 wameuwawa na nusu ya wakaazi wamekimbia makaazi yao.
Lakini ghasia zimeendelea, zikiakisi misimamo tofauti baina ya mataifa hayo matatu, ambayo bila ya kuwepo kwa uingiliaji kati wa mataifa ya magharibi, wanashikilia mustakabali wa Syria kwa kiasi kikubwa katika mikono yao.
Jeshi la Syria na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran , wakiwa na msaada wa ndege za kivita za Urusi, wamekandamiza wapinzani karibu na mji mkuu Damascus katika eneo la Ghouta Mashariki moja kati ya maeneo manne yanayoelezewa kama ni kanda zitakazokuwa hazina shughuli za kijeshi.
Uturuki yashutumu na kufanya mashambulizi
Uturuki , ambayo ilishutumu vikali mashambulizi dhidi ya Ghouta mashariki , ilifanya operesheni nayo ya kijeshi kuwaondoa wapiganaji wa Kikurdi wa YPG kutoka katika jimbo la kaskazini magharibi la Afrin. Uturuki imeahidi kuukamata mji wa Tel Rifaat na kuendelea zaidi upande wa mashariki, na kuikasirisha Iran.
"Pamoja na nia iliyopo, hatua za Uturuki nchini Syria , iwapo ni Afrin, Tel Rifaat na maeneo mengine ya Syria, yanapaswa kusitishwa haraka iwezekanavyo," afisa mwandamizi wa Iran amesema.
Iran imekuwa mshirika ambaye ametoa usaidizi mkubwa kwa rais Assad wakati wote wa mzozo huo. Wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwanza walilisaidia jeshi lake kuwazuwia waasi kusonga mbele, wakifuatiwa na kuingia kwa Urusi katika vita hivyo mwaka 2015, na kubadilisha wimbi kuelekea upande wa Assad.
Rais Vladimir Putin amewasili leo mjini Ankara kushiriki katika sherehe za kuanza ujenzi wa kinu cha kwanza cha kinyuklia kitakachotumika kutoa nishati na mkutano kuhusu Syria kesho Jumatano. Hii ni ziara ya kwanza ya Putin nje ya nchi tangu kuchaguliwa tena mwezi uliopita. Alikutana na rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki mara nane mwaka 2017 wakati uhusiano baina ya nchi hizo mbili ulipoanza kuimarika kukiwa na ushirikiano wa masuala ya nishati na pia ndani ya Syria, na wakati Uturuki ikikabili hali ngumu katika uhusiano wake na mataifa ya magharibi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman