Urusi kumuhamishia Navalny hospitali baada ya kushinikizwa
19 Aprili 2021Taarifa zaidi zinasema kwamba Navalnyatapelekwa katika hospitali ya wafungwa katika mji ulioko mashariki mwa Moscow na kwamba afya yake ni ya "kuridhisha" na amekubali kumeza madawa.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, wanatarajiwa kukutana leo kwa njia ya video kujadili afya ya mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi Alexei Navalny, ambaye washirika wake wa karibu wanadai kuwa yumo katika hali mbaya gerezani.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema hii leo kwamba Urusi inapaswa kumruhusu Navalny kupatiwa matibabu sahihi wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wakijiandaa kushiriki mazungumzo kwa njia ya vidio kuhusu afya ya mwanasiasa huyo.
Borrell amenukuliwa akisema kuwa hali ya kiafya ya mwanasiasa huyo ni ya "kutia mashaka" na kwamba "Urusi inawajibika kwa ajili ya afya ya Navalny".
"Tuna wasiwasi na hali ya afya ya mkosoaji wa Urusi bw. Navalny. Jana tulitoa kauli kwa niaba ya wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya, tukizitaka mamlaka za Urusi kumpatia matibabu anayohitaji. wanawajibika kwa ajili ya usalama wake."
Navalny mwenye umri wa miaka 44 na mkosoaji mkubwa wa rais wa Urusi Vladmir Putin alitangaza mgomo wa kula mwishoni mwa mwezi Machi katika kupinga kile alichokielezea kuwa ni mamlaka za magereza kukataa kumpatia matibabu sahihi ya mgongo na maumivu ya mguu.
Kabla ya mkutano wa leo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya jana walitoa kauli ya pamoja wakionya juu ya maisha ya Navalny kuwa hatarini.
Marekani nayo imeionya Ikulu ya Urusi Kremlin juu ya "madhara" yatakayojitokeza endapo mwanasiasa huyo atafariki akiwa gerezani. Kauli hiyo ilitolewa baada ya madaktari kuonya mwishoni mwa juma kwamba Navalny anaweza kufariki "dakika yoyote".
Wasiwasi juu ya afya ya Navalny unakuja katikati mwa hofu kubwa kufuatia hatua ya Urusi kupeleka wanajeshi katika mpaka wake na Ukraine na pia kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia baina ya Moscow na mwanachama wa Umoja wa Ulaya Jamhuri ya Czech.
Mwanasiasa huyo ambaye nchi za magharibi zinadai kuwa alifungwa jela kimakosa na kwamba lazima aachiwe huru, alirejea Urusi mnamo mwezi Januari baada ya kupatiwa matibabu nchini Ujerumani kufuatia madai ya kulishwa sumu.
Washirika wawili wa karibu wa Navalny, Vladimir Ashurkov na Leonid Volkov, wamewaandikia barua mawaziri wa Umoja wa Ulaya wakiwaomba kushiriki mkutano wa leo katika kujadili afya ya mwanasiasa huyo.
Barua hiyo inaelezea wasiwasi wa kiafya sawa na ule uliotolewa na mke wa Navalny siku ya Jumanne baada ya kumtembelea jela na kudai kwamba anapata ugumu katika kuzungumza na amepoteza uzito mkubwa.