Urusi kupeleka silaha zaidi kwa wanajeshi walioko Ukraine
1 Aprili 2023Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, ametembelea makao makuu ya wanajeshi wa Moscow wanaopigana nchini Ukraine leo, na kuahidi kuongeza silaha kwa vikosi vya Urusi vilivyoko katika uwanja wa vita.
Katika video iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Urusi kupitia mtandao wa Telegram, Shoigu ameonekana akiongoza mkutano na maafisa waandamizi wa kijeshi akiwemo Jenerali Valery Gerasimov, mmoja wa askari wa ngazi ya juu wa Urusi.
Shoigu amekabiliwa na ukosoaji mkali kwa kushindwa kusambaza silaha za kutosha kwa wanajeshi walioko uwanja wa mapambano.
Wakati huo huo, Urusi inatarajiwa hii leo kuchukua urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi wa Aprili. Siku moja kabla, Ikulu ya Urusi Kremlin ilisema kwamba Urusi itatekeleza haki zote zinazoendana na jukumu hilo.