1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi kuzingatia juhudi za amani za Afrika

28 Julai 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewaambia viongozi wa Afrika Ijumaa kwamba nchi yake inaheshimu pendekezo lake la amani katika vita dhidi ya Ukraine na inalitazama kwa makini.

Russland, Sankt Petersburg | Zweiter Wirtschafts- und humanitärer Gipfel 2023, Russland - Afrika | Wladimir Putin, Präsident
Picha: Pavel Bednyakov/POOL/AFP/Getty Images

"Tuchukue kwa mfano juhudi za mataifa kadhaa ya Afrika kuutatua mzozo wa Ukraine. Hili ni tatizo kubwa na hatukwepi kulizingatia kwasababu zamani, juhudi za kuleta amani zilikuwa zimetengewa tu nchi zinazosemekana kwamba zimeendelea kidemokrasia. Sasa Afrika nayo iko tayari kusaidia kuhusiana na matatizo yanayoonekana kuwa nje ya eneo lake kuu la maslahi. Tunaheshimu juhudi zenu," alisema Putin.

Rais Putin ametoa tamko hilo katika siku ya pili ya mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika unaofikia kilele chake Ijumaa huko Saint Petersburg. Mwezi Juni viongozi wa Afrika waliwasilisha mpango wao wa amani kwa Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ila mpango huo ulionekana kutotiliwa maanani na viongozi hao.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji (kushoto) akiwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi (kulia)Picha: Alexei Danichev/REUTERS

Afrika kupewa silaha za kuimarisha usalama na Urusi

Awali Putin aliupokea mpango huo kisha akataja malalamiko aliyo nayo kwa Ukraine na mataifa ya Magharibi. Zelenskiy kwa upande wake amekataa wazo la usitishwaji wa mapigano utakaoipelekea Urusi kudhibiti sehemu kubwa ya Ukraine na kulipa nafasi jeshi lake kujipanga upya.

Katika mkutano huo huo wa kilele kati ya Urusi na Afrika, Putin amesema nchi yake iko tayari kuipa Afrika silaha bila malipo kwa ajili ya kuimarisha usalama katika bara hilo. Fauka ya hayo, kiongozi huyo amesema yuko tayari kufanya kazi na walinda usalama wa Afrika na mashirika ya ujasusi. Ameongeza kwamba urusi imeyafuta madeni ya nchi kadhaa za Afrika ambazo hakuzitaja, ya kima cha dola bilioni 23.

Hayo yakiarifiwa, mamlaka za Ukraine zinasema mtu mmoja amefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa kufuatia mashambulizi ya maroketi usiku kucha, katika miundo mbinu ya bandari katika eneo la Odessa.

Jeshi la Ukraine vile vile limesema limezua mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani katika maeneo ya Dnipropetrovsk na Donetsk. Urusi inadaiwa kukutuma makombora mawili ya Kalibr na droni 8 za kamikaze.

Urusi yapigwa na vikwazo zaidi vya Japan

Hapo Alhamis Rais Putin alidai kwamba jeshi la Ukraine halijapata mafanikio yoyote licha ya kuzidisha mashambulizi katika siku za hivi karibuni.

Athari za vita vya Ukraine kwa watumiaji wa ngano Afrika

02:40

This browser does not support the video element.

Haya yanafanyika wakati ambapo Japan imeongeza vikwazo dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, vikwazo hivyo vikijumuisha marufuku ya kuiuzia Urusi magari ya kielektroniki.

Vikwazo hivyo vipya vilivyoidhinishwa na baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Fumio Kishida Ijumaa, vitaanza kutekelezwa Agosti 9.

Vikwazo hivi vya Japan kwa Urusi, vinafuatia vyengine kama nhivyo vilivyotangazwa na Marekani na Umoja wa Ulaya.

Vyanzo: AFP/DPAE/Reuters