Urusi: Maelfu wakusanyika kumzika Mikhail Gorbachev
3 Septemba 2022Hata hivyo mazishi yake hayakuwa ya kiserikali. Gorbachev amezikwa mahala ambapo viongozi wa hapo awali wa Umoja wa Kisoviet wamezikwa ikiwa pamoja na Lenin, Stalin na Brezhnev.
Rais wa Urusi Vladmir Putin hakuhudhuria mazishi ya Gorbachev na amesema kusambaratika kwa Umoja wa Kisoviet ni maafa makubwa ya siasa za kikanda. Hata hivmnamo siku ya Alhamisi kwa faragha, rais Putin aliweka shada la maua kwenye jeneza la Gorbachev katika hospitali ambako alifariki. Makamu wa rais wa Urusi Dmitry Medvedev alihudhuria mazishi hayo.Viongozi wa nje waliohudhuria walikuwa pamoja na waziri mkuu wa Hungary Victor Orban na wawakilishi wa kibalozi.
Baadhi ya watu wanamlaumu Gorbachev kwa kuanzisha mageuzi yaliyosababisha vurumai za kiuchumi na pia kusababisha kusambaratika kwa Umoja wa Kisoviet. Hata hivyo marehemu kiongozi huyo anaheshimiwa miongoni mwa nchi za magharibi kwa kwa kuanzisha sera zilizovimaliza vita baridi barani Ulaya. Wajerumani ndiyo walionufaika kwa kiwango kikubwa na sera za Gorbachev. Ujerumani iliyogawanywa baada ya kumalizika vita vikuu vya pili iliweza kuungana tena.
Mikhail Gorbachev aliingia madarakani mnamo mwaka 1985 na kuanza kujenga ujasiri wa kuleta mageuzi. Hakuna kiongozi mwingine wa Umoja wa Kisoviet wa hapo awali aliyethubutu kupitia njia hiyo. Hata hivyo hakuweza kuepusha kusambaratika kwa umoja huo.
Nchi zilizokuwamo katika umoja huo zilianza kujitangazia uhuru. Hadi kufika mwaka 1991 Umoja wa Kisoviet ulikata roho. Hata hivyo nje ya Urusi Gorbachev aliheshimiwa kwa kiwango kikubwa.Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Gorbachev aliubadilisha mkondo wa historia. Rais wa Marekani Joe Biden amemwita Gorbachev kuwa kiongozi adimu.
Gorbachev alifariki Jumanne iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu.Alitimiza umri wa miaka 91. Hayati kiongozi huyo mashuhuri amezikwa karibu na kaburi la mkewe Raisa, kwenye maziara ya Novodevichy mjini Moscow.
Vyanzo:/AP/RTRE