Urusi: Mashambulio ya droni kuilenga Moscow hayakufanikiwa
21 Agosti 2024Wizara ya ulinzi ya Urusi imeeleza kuwa mfumo wake wa ulinzi wa anga uliharibu droni 11 katika mji mkuu Moscow na maeneo yaliyo karibu na jiji hilo.
Meya wa jiji la Moscow Sergei Sobyanin, amesema hili ni moja kati ya majaribio makubwa kuwahi kutokea la kutaka kuushambulia mji wa Moscow kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Meya huyo amesema katika mashambulio hayo ya usiku wa kuamkia leo hakuna uharibifu au hasara yoyote iliyotokea.
Majaribio ya Ukraine ya hivi karibuni ya kuulenga mji mkuu wa Urusi, Moscow ni makubwa kuliko mashambulio ya mwezi Mei mwaka jana.
Soma Pia: Ukraine, Urusi zadai kuimarisha mashambulizi
Mashambulizi hayo ya droni yanafanyika huku vikosi vya Ukraine vikiendelea kupambana katika eneo la Kursk Magharibi mwa Urusi.
Idara ya sera ya Taasisi inayofanya utafiti wa vita, iliyoko Washington, Marekani imesema katika ripoti yake ya kila siku kwamba jeshi la Ukraine limepiga hatua na kupata ufanisi wa ziada katika operesheni yake ya sasa, ambayo imeingia katika wiki yake ya tatu.
Taasisi hiyo imebainisha kuwa vikosi vya Ukraine vimefaulu kuyalipua madaraja na vifaa vya uhandisi vya Urusi kwenye Mto Seym katika eneo la magharibi mwa mkoa wa Kursk na kwamba mafaniko hayo yameongeza ujasiri na ari nchini Ukraine kwamba sasa nchi hiyo imefaulu kuubadilisha muelekeo wa mapigano kati yake na Urusi.
Soma Pia: Urusi na Ukraine zaendelea kupambana vikali huko Kursk
Lakini taasisi hiyo imekumbusha kuwa wakati Ukraine inafurahia ushindi wa upande mmoja nchi hiyo inaendelea kupoteza ardhi katika kanda yake ya mashariki iliyo na viwanda.
Naibu mkuu wa baraza la usalama la Urusi, Dmitry Medvedev, amesema leo Jumatano kwamba uvamizi wa Ukraine katika eneo la Kursk ndani ya ardhi ya Urusi unamaanisha kuwa mazungumzo ya kuvimaliza vita kati ya Moscow na Kyiv hayatakuwepo hadi Urusi itakapoishinda Ukraine ikwenye uwanja wa vita.
Kwa upande wake kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov alipokutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin anayefanya ziara yake ya kwanza katika eneo hilo tangu mwaka 2011 kwamba eneo lake limepeleka wapiganaji zaidi 47,000 katika eneo la mzozo kati ya Urusi na Ukraine.
Soma Pia: Urusi bado yapambana na wanajeshi wa Ukraine waliovuka mpaka
Naye Sergei Chemezov, mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema kuna hatari kubwa ya kusababisha vita vitakavyozagaa duniani iwapo Marekani na washirika wake wa Magharibi wataendelea kuchochea migogoro nchini Ukraine na kuruhusu majeshi ya Ukraine kushambulia ndani ya Urusi.
Vyanzo: RTRE/AP