1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, mataifa ya Magharibi wabadilishana wafungwa

Angela Mdungu
2 Agosti 2024

Zoezi kubwa la kubadilishana wafungwa limefanyika jana Alhamisi kati ya Urusi na mataifa kadhaa ya magharibi yakiwemo Ujerumani na Marekani. Katika mchakato huo wafungwa 26 waliachiliwa huru na Urusi

Ubadilishanaji wafungwa Urusi, mataifa ya magharibi
Raia wa Marekani walioachiliwa huru na Urusi wakiwasili MarekaniPicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Marekani na Urusi zimekamilisha shughuli ya kubadilishana wafungwa, baada ya Moscow kuwaachilia mwandishi wa habari Evan Gershkovich, mwanajeshi wa zamani wa majini wa Uingereza  Paul Whelan pamoja na baadhi ya wakosoaji wa Urusi akiwemo mwanaharakati mwenye uraia wa Urusi na Uingereza Vladimir Kara-Murza. Alsu Kurmasheva, mwandishi wa habari mwenye uraia pacha wa Urusi na Marekani pia aliachiliwa huru.

Soma zaidi: Urusi yakamilisha mpango wa kubadilishana wafungwa na Magharibi

Wafungwa hao walioachiliwa na Urusi waliwasili Marekani majira ya usiku na kuungana na familia zao. Walipokelewa na Rais wa Joe Biden na makamu wake Kamala Harris aliyemsifu Biden kwa namna alivyoshirikiana na mataifa washirika na kufanikisha zoezi hilo.

Nchini Ujerumani, katika uwanja wa ndege wa Cologne/Bonn ndege mbili zilizokuwa zimewabeba watu 13 ziliwasili kutoka Ankara ambako ndipo ubadilishanaji huo wa wafungwa ulifanyika.

Soma zaidi: Urusi yamhukumu kifungo cha miaka 16 mwandishi wa Marekani

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ndiye aliyewapokea wafungwa hao walioachiliwa ambapo alisema wengi wao hawakuitarajia hatua hiyo. Sharti la kuachiliwa kwa wafungwa hao wa Ujerumani, Marekani na nchi washirika lilikuwa ni kuwaachilia wafungwa wenye uraia wa Urusi waliozuiwa kwenye mataifa hayo kwa tuhuma za ujasusi.

Wafungwa wa Urusi walioachiliwa huru wakiwasili Moscow Picha: Sergei Ilyin/AP

Aliyefungwa maisha jela aachiliwa na Ujerumani

Ujerumani kwa upande wake ililazimika kumuachia huru Vadim Krasikov, aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la mauaji ya raia wa Chechnya mchana kweupe mjini Berlin mwaka 2019.

Upande wa pili, Warusi nane waliachiliwa huruna kupewa mapokezi ya kihistoria na Rais Vladimir Putin. Kiongozi huyo amewaahidi wafungwa hao walioachiliwa kuwapa tuzo za kitaifa na atafanya nao mazungumzo kuhusu mustakabali wa maisha yao.

Miongoni mwao ni wanaume wawili Vladislav Klyushin na Roman Seleznyov waliokuwa wakitumikia kifungo Marekani kwa makosa ya uhalifu wa mtandaoni. Makubaliano ya kubadilishana wafungwa hao yalifikiwa baada ya majadiliano ya siri ya zaidi ya mwaka mmoja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW