1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Mazungumzo na Ukraine hayatositisha mashambulizi

27 Februari 2022

Serikali Urisi imeionya Ukraine kwamba operesheni za kijeshi hazitasimamishwa katika mazungumzo yoyote yanayowezekana kufanyika. Tarifa hiyo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, Interfax.

Russland Region Belgorod | Militärfahrzeuge in der Grenzeregion zur Ukraine
Picha: Mikhail Voskresenskiy/SNA/imago images

Urusi awali ilisema ujumbe wake uko tayari kukutana na wa serikali ya Ukraine katika mji wa Gomel nchini Belarus, eneo ambalo limekataliwa na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky akisema serikali ya Minsk yenyewe imehusika katika uvamizi wa Urusi.

Hata hivyo, katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya mtandao amesema yupo tayari kwa mazungumzo na kutoa mapendekezo ya miji ya Warsaw, Bratislava, Budapest, Istanbul na Baku.

Mazungumzo ya kuaminika kumaliza vita

Rais huyo mwenye umri wa miaka 44 amesema pia hata katika eneo lolote ambalo makombora yake hayawezi kurushwa litakuwa eneo zuri kwa mazungumzo na kwa namna hiyo mazungumzo yatakuwa ya kuaminika, na kumaliza vita.

Alhamisi iliyopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin, alianzisha mashambulizi kamili dhidi ya Ukraine ambayo hadi wakati huu yamegharimu maisha ya takribani watu 200 na kulaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep BorrellPicha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kufanya mkutano Jumapili, katika juhudi yao ya kuitikia wito wa dharura wa serikali ya Ukraine wa kutoa msaada wa kijeshi na kuzidisha vikwazo dhidi ya Urusi baada ya kuivamia Ukraine.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba watafanya mkutano kwa njia ya vidio baadae leo, ikiwa ni siku ya nne tangu Urusi iivamie Ukraine, hatua ambayo pia imesababisha Rais Putin alengwe na vikwazo binafsi.

Umoja wa Ulaya kuiunga mkono Ukraine

Borrell amesema mkutano huo utakuwa wa kuidhinisha hatua zaidi za kuiunga mkono Ukraine, dhidi ya uvamizi wa Urusi na kwamba yeye atatoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya misaada ya dharura kwa jeshi la Ukraine ili kuunga mkono katika kile alichokiita mapambano yao ya kishujaa.

Pamoja na mambo mengine Rais Zelensky amerejea mara kadhaa kuuomba Umoja wa Ulaya kuizuia Urusi katika mfumo wa malipo ya kibenki wa kimataifa wa SWIFT hatua ambayo tayari ilionesha athari kubwa kwa Iran, pale ilipoadhibiwa kutokana na mpango wake ya nyuklia.

Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Ama kwa upande mwingine Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz Jumapili atalihutubia bunge katika kikao maalum kwa lengo la kutolea ufafanuzi kuifanyia mabadiliko sera iliyodumu kwa miaka kadhaa ya usafirishaji silaha, pamoja na kuruhusu upelekwaji wa silaha wa moja kwa moja nchini Ukraine.

Siku ya Jumamosi serikali ya Ujerumani ilitoa uamuzi wa kuwapelekea silaha kwa haraka iwezekanavyo wanajeshi wa Ukraine. Silaha zilizoainishwa katika hatua hiyo kutoka katika jeshi la Ujerumani ni kiasi cha 1,000 zile za kujikinga na vifaru pamoja na makombora 500 ya ardhini hadi angani. Tangazo hilo lilipongezwa mara moja na Rais Zelensky.

Hotuba ya Kansela Scholz inasukumwa na rekodi inayoonesha Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikijitenga kisera kusafirisha silaha zozote katika eneo la vita, au kuruhusu nchi nyingine ya pembeni kupeleka silaha zilizotengenezwa na Ujerumani katika maeneo hayo.

 

(AFP, DPA, Reuters)

   

   

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW