1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi na Belarus zasaini makubaliano ya silaha

25 Mei 2023

Urusi na Belarus zimetia saini makubaliano ya kurasimisha mpango wa kupeleka silaha za nyuklia nchini Belarus.

Moskau Treffen Putin (R) und Li Shangfu Verteidigungsminister China
Picha: PAVEL BEDNYAKOV/SPUTNIK/AFP

Hatua hiyo inafuatia makubaliano ya awali yaliyofikiwa na Rais Vladimir Putin na mwenzake wa Belarus, Alexander Lukashenko. 

Mnamo mwezi Machi, Rais Putin alitangaza kwamba nchi yake inapanga kupeleka silaha za nyuklia za kimkakati na masafa mafupi nchini Belarus. Na sasa kutiwa saini makubaliano hayo kunafanyika wakati ambapo Urusi inajiandaa kwa mashambulizi ya kulipa kisasi dhidi ya Ukraine. Maafisa wa Urusi na Belarus wanasema hatua hiyo imetokana na chuki za nchi za Magharibi.

Soma pia: Ukraine yadai imezuia mashambulizi ya droni ya Urusi

Akizungumza baada ya kutiwa saini makubaliano hayo Waziri wa Ulinzi wa Belarus, Viktor Khrenin, amesema: "Ndani ya mfumo wa ushirikiano wa kijeshi na kiufundi kati ya nchi zetu, hatua zimechukuliwa ili kujenga uwezo wa kupambana na kikundi cha askari wa kikanda, hasa, kuwapa silaha mpya za kisasa.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, amepongeza kile alichokiita ushirikiano wa nchi hizo mbili: "Jamhuri ya Belarus imekuwa na inabakia kuwa mshirika wetu wa kweli na wa kuaminika. Leo, tunasimama pamoja dhidi ya nchi za Magharibi kwa pamoja, ambayo, kwa kweli, inaongoza vita visivyojulikana dhidi ya nchi zetu."

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na lini silaha hizo zitakapopelekwa ila Rais Putin alisema kuwa ujenzi wa hifadhi za silaha hizo utaanza huko Belarus tarehe Mosi Julai. Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni, Svetlana Tsikhanouskaya, amelaani hatua hiyo.

Soma pia: Urusi yaituhumu Marekani kupanga shambulizi ikulu ya Kremlin

Huku haya yakijiri, serikali ya Finland imesema leo Alhamis itatuma zana za ziada za kijeshi kwa Ukraine, pamoja na silaha za kujikinga na mashambulizi ya ndege na risasi zenye thamani ya euro milioni 109 sawa na dola milioni 120.

Uwanja wa mapambano

Katika uwanja wa mapambano, Ikulu ya Kremlin imeishutumu Ukraine kwa kupanga kushambulia nyaya zinazosambaza umeme wa kiwango cha juu katika vinu viwili vya nguvu za nyuklia kaskazini mwa Urusi.

Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema hayo alipotoa maoni yake kupitia shirika la habari la Urusi la Interfax kuhusu ripoti za ujasusi wa ndani ya FSB baada ya kukamatwa watu wawili wanaodaiwa kutaka kuripua nyaya zinazosambaza umeme wa kiwango cha juu katika mitambo ya nyuklia ili kusitisha shughuli za mitambo hiyo.

Kwengineko, mkuu wa kundi la mamluki la Wagner la Urusi, Yevgeny Prigozhin, amesema kwamba vikosi hivyo vimeanza kujiondoa katika mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine ili kupumzika na kujiandaa kupelekwa katika maeneo mengine. 

Soma pia: Zelenskiy amesema Bakhmut bado inadhibitiwa na Ukraine

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar, amethibitisha kujiondoa kwa kundi la Wagner na kwamba walikuwa wakibadilishwa na wanajeshi wa kawaida wa Urusi na kuongezea kuwa vikosi vya Ukraine vinaendelea kudhibiti eneo la kusini-magharibi mwa Bakhmut.