Urusi, China zapinga mashambulizi ya Marekani na UK Yemen
15 Februari 2024Urusi na China zimezituhumu Marekanin na Uingereza kwa kuyashambulia kinyume cha sheria maeneo ya kijeshi yanayotumiwa na waasi wa Houthi wa Yemen kurusha makombora dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu na kutatiza safari za meli duniani.
Naibu balozi wa Marekani Robert Wood na balozi wa Uingereza Barbara Woodward wamepinga wakisema mashambulizi ya Wahouthi ni kinyume cha sheria, na hatua zao ambazo ni za kisheria dhidi ya waasi hao wa Yemen zinachukuliwa kujilinda.
Soma pia: Wahouthi washambulia meli nje ya pwani ya Kusini mwa Yemen
Woodward alisema mashambulizi ya Wahouthi yanasababisha kupanda kwa gharama ya usafirishaji wa meli, zikiwemo gharama za bidhaa za chakula na msaada wa kiutu katika kanda hiyo.
Lakini Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dimtry Polyansky na balozi wa China Zhang Jun wamehoji kuwa Baraza la Usalama halijawahi kuidhinisha hatua ya kijeshi dhidi ya Yemen.
Makabiliano hayo yalitokea katika mkutano wa baraza ambapo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Hans Grundberg alisema juhudi za kurejesha amani Yemen zinatatizwa na kuongezeka kwa mivutano ya kikanda, hasa vita vya Gaza na mashambulizi ya kijeshi katika Bahari ya Shamu.