1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zampongeza Assad kwa kuchaguliwa tena

28 Mei 2021

Siku ya Ijumaa Urusi imempongeza rais wa Syria Bashar al- Assad baada ya kudai ushindi wa kura nyingi katika uchaguzi wa nchi hiyo ambao umekashifiwa na upinzani na Mataifa ya Magharibi.

BG Wahl in Syrien
Rais Bashar al-Assad wa Syria akipiga kura huko mjini Douma, Syria katika uchaguzi uliofanyika Jumatano ya wiki hiiPicha: SANA/REUTERS

Katika taarifa kupitia wizara yake ya mambo ya nje, Urusi imesema kuwa rais wa sasa wa nchi hiyo al-Assad ameshinda katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa wanachukulia uchaguzi huo kama suala la uhuru wa Jamhuri hiyo ya Kiarabu ya Syria na hatua muhimu katika kuimarisha udhibiti wa ndani wa taifa hilo.

Taarifa hiyo, ilifafanua matamshi ya Magharibi yanayotilia shaka uhalali wa uchaguzi huo kama "jaribio lingine la kuingilia masuala ya ndani ya Syria kwa lengo la kuyadumaza.''

Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa hakuna mtu aliye na haki ya kuwaamuru Wasyria ni lini na chini ya hali gani wanapaswa kumchagua rais wao.

Urusi imekuwa mshirika muhimu kwa utawala wa Syria katika mzozo nchini humo na uingiliaji wake katika vita mnamo Septemba 2015 ulionekana kuwa imegeuza wimbi la mapigano kwa kumpendelea  Assad

China yampongeza Assad

Siku ya Ijumaa, China pia ilituma risala zake za pongezi kwa rais Bashar al-Assad kwa kushinda muhula wa nne uongozini.

Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Ijapokuwa anakashifiwa na Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza, kiongozi huyo ya Syria anaendelea kufurahia uungwaji mkono kutoka kwa China.

Wakati wa kikao na wanahabari siku ya Ijumaa mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Zhao Lijian, amesema kuwa Syria na China ni washirika wa karibu wa jadi na kwamba taifa hilo linaiunga mkono kikamilifu Syria katika kulinda uhuru wake na uadilifu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW