1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Urusi, China zaishutumu Marekani na Uingereza kuhusu Wahuthi

Sylvia Mwehozi
15 Februari 2024

Urusi na China zimeishutumu Marekani na Uingereza kwa kuyashambulia kinyume cha sheria maeneo ya kijeshi yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi wa Yemen.

Umoja wa Mataifa
Baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: Eskinder Debebe/UN Photo/picture alliance/Xinhua News Agency

Urusi na China zimeishutumu Marekani na Uingereza kwa kuyashambulia kinyume cha sheria maeneo ya kijeshi yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi wa Yemen, wanaozishambulia meli za biashara katika Bahari ya Shamu.

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Robert Wood na Balozi wa Uingereza Barbara Woodward wamepinga shutuma hizo, wakisema mashambulizi dhidi ya waasi ni hatua za kisheria na sahihi, na za kujilinda.

Hata hivyo, naibu balozi wa Urusi Dmitry Polyansky na mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun walidai kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kamwe halikuidhinisha hatua za kijeshi dhidi ya Yemen.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Hans Grundberg amelieza baraza la usalama kwamba juhudi za kurejesha amani nchini Yemen, zimedhoofishwa na kuongezeka kwa mvutano wa kikanda.