1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Urusi na China zatofautiana na Marekani na Uingereza

15 Februari 2024

Urusi na China zimeishutumu Marekani na Uingereza kwa kuyashambulia kinyume cha sheria maeneo ya kijeshi yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi wa Yemen.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood (kulia) na Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Barbara Woodward (kushoto) wahudhuria mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Picha: CHARLY TRIBALLEAU/AFP/Getty Images

Kurusha makombora kwenye meli za biashara katika Bahari ya Shamu na kutatiza usafirishaji wa kimataifa. 

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Robert Wood na Balozi wa Uingereza Barbara Woodward wamepinga shutuma hizo, wakijibu kwamba mashambulizi dhidi ya waasi Kihouthi ni hatua sahihi kisheria na za kujilinda.

Soma pia: Wahouthi washambulia meli nje ya pwani ya Kusini mwa Yemen

Woodward ameongeza kusema kwamba mashambulizi ya Wahouthi "yanaongeza gharama za kimataifa za usafirishaji wa meli, pamoja na gharama za chakula na misaada ya kibinadamu katika eneo hilo."

Hata hivyo, naibu balozi wa Urusi Dmitry Polyansky na mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun walidai kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kamwe halikuidhinisha hatua za kijeshi dhidi ya Yemen.

Juhudi za amani 

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg.Picha: Fayez Nureldine/AFP

Majibizano yaliibuka katika kikao cha baraza hilo ambapo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg alisema kuahidi juhudi za kurejesha amani Yemen kumepungua kutokana na kuongezeka kwa mvutano wa kikanda unaohusishwa na vita vya Gaza.

Soma pia: Waasi wa Houthi wasema wataanza kuzilenga meli za Marekani

Grundberg alisema "Kuongezeka kwa mvutano wa kikanda unaohusishwa na vita huko Gaza, na haswa kuongezeka mashambulizi ya kijeshi katika Bahari ya Shamu, kunapunguza kasi ya juhudi za amani huko Yemen.

"Kadri nilivyojaribu kuuweka   mchakato wa amani katika mtazamo  mpana  wa kikanda, ukweli ni kwamba juhudi za upatanishi nchini Yemen haziwezi kuzuiwa. Matukio ya kikanda huathiri Yemen, na kinachotokea Yemen kinaweza kuathiri eneo zima. Aliongezea Grundberg.

Tangu mwezi Novemba, waasi wa Kihouthi wamelenga meli katika Bahari ya Shamu katika juhudi za kushinikiza kusitishwa kwa mapigano katika mashambulizi ya Israel huko Gaza. Mara kwa mara wamekuwa wakizishambulia meli zenye uhusiano na Israeli, na kuharibu usafiri wa meli katika njia kuu ya biashara kati ya Asia, Mashariki ya Kati na Ulaya.

Huku haya yakijiri Iran imesema itajibu ikiwa meli zake zitakamatwa, hii baada ya Wizara ya Sheria ya Marekani mapema mwezi huu kutangaza kwamba imekamata zaidi ya mapipa 500,000 ya mafuta ya Iran ili kubana kile walichokitaja kama "mtandao wa ufadhili wa walinzi wa mapinduzi."

 

//Reuters, AP