1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zatumia kura ya turufu kuzuia msaada wa Syria

8 Julai 2020

Urusi na China zimetumia kura ya turufu kulipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingeongeza muda wa mwaka mmoja zaidi msaada wa kibinaadamu kupelekwa Syria kutoka Uturuki.

Syrien: Rotes Kreuz im Konfliktgebiet
Picha: Getty Images/AFP/A. Almohibany

Ujerumani na Ubelgiji, nchi mbili ambazo sio wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ziliwasilisha azimio hilo ambalo lingeruhusu msaada kuendelea kupelekwa Syria kupitia vituo viwili vya kuvukia katika mpaka wa Uturuki bila ya serikali ya Syria kuingilia kati.

Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Christoph Heusgen, rais wa baraza hilo kwa mwezi huu, amesema rasimu ya azimio hilo haijapitishwa na kuongeza kuwa mbali na Urusi na China, nchi 13 wanachama wa baraza hilo zilipiga kura kuipitisha rasimu ya azimio hilo.

Mara tu baada ya kura hiyo, Urusi ilipendekeza azimio lake ambalo linataka muda utakaoongezwa usizidi miezi sita na kwamba msaada huo uruhusiwe kupitia kwenye eneo moja tu la mpaka kati ya Syria na Uturuki na sio vituo viwili. Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia amesema nchi hiyo inataka kituo cha Bab al-Salam kiondolewe kwenye utaratibu huo.

Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Christoph HeusgenPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/A. Ozdil

''Tunahitaji kuendelea kuutumia mpaka wa kaskazini magharibi. Na kwa minajili hiyo tunajaribu kuelezea jinsi tunavyoona uratibu huu unaweza kuendelea. Azimio lililopendekezwa halikupitishwa, lakini sisi tumewasilisha rasimu yetu ambayo tumeisambaza hivi karibuni,'' alifafanua Nebenzia.

Matokeo ya kura kuhusu azimio hilo yatajulikana baadae siku ya Jumatano. Urusi mshirika wa karibu wa Rais wa Syria Bashar al-Assad, inataka utoaji wa msaada wa kibinaadamu uwe chini ya udhibiti ya serikali ya Syria. Idhini ya kupelekwa msaada wa kibinaadamu kwa kuvuka mipaka imekuwepo tangu mwaka 2014, na muda wa kufanya hivyo umekuwa ukiongezwa mara kwa mara. Azimio lililopitishwa kuidhinisha utoaji wa msaada wa sasa linamalizika siku ya Ijumaa.

China na msimamo wake

Baada ya kura hiyo, Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Zhang Jun amesema wanaunga mkono kuongezwa muda wa utoaji misaada kupitia mipakani, lakini Ujerumani na Ubelgiji zimekataa kulizingatia ombi lake la kulaani vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya vilivyowekwa dhidi ya Syria.

Katika kura ya Jumanne, Urusi iliitumia kura yake ya turufu kwa mara ya 15 tangu kuzuka kwa vita vya Syria mwaka 2011, huku China ikiitumia kura yake ya turufu kwa mara ya tisa.

Katika ripoti yake ya mwezi Juni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kuongezwa kwa muda wa mwaka mmoja utoaji wa misaada ya kibinaadamu kupitia vituo viwili vya mpakani. Guterres amesema tangu mwaka 2014, malori 4,774 yamekitumia kituo cha Bab al-Salam kuvuka mpaka na malori 28,574 yamekitumia kituo cha Bab al-Hawa.

Lori la Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC likipeleka misaada SyriaPicha: Getty Images/AFP/M. Taha

Urusi na China zimepiga kura ya turufu, licha ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa maisha ya raia wa Syria yanategemea msaada unaoingia kupitia mipakani. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mjini Geneva siku ya Jumanne, hali ya kibinaadamu kwenye jimbo la Idlib ni mbaya na uchumi wa Syria umeporomoka.

Juni 29, mkuu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba takriban watu milioni 2.8 kaskazini magharibi mwa Syria wawanahitaji msaada wa kibinaadamu. Lowcock amesema mwezi Aprili, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP lilipeleka msaada wa chakula kwa watu milioni 1.3 kupitia vituo viwili vya mpakani na mwezi Mei Shirika la Afya Duniani, WHO lilipeleka vifaa vya afya vya dharura 420,000 pamoja na dawa kwenye eneo la kaskazini magharibi.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW