1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Iran kutia saini mkataba mpya wa ushirikiano

17 Januari 2024

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema, inatarajia hivi karibuni Rais Vladimir Putin na mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi watatia saini mkataba mpya wa ushirikiano ambao uko katika hatua za mwisho za kukubaliwa.

Ebrahim Raisi na Wladimir Putin
Rais wa Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Urusi Vladimir PutinPicha: Alexandr Demyanchuk/AP/picture alliance

Mwezi uliopita, Putin alifanya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tano katika ikulu ya Kremlin na Ebrahim Raisi katikati ya ongezeko la ushirikiano wa kisiasa, kibiashara na kijeshi kati ya Moscow na Tehran, ushirikiano ambao unawatia wasiwasi Marekani na Israel.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharov amewaambia waandishi wa habari kwamba, makubaliano hayo yataimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Tehran.

Bi. Zakharov amesema tangu kusainiwa kwa mkataba wa sasa, mazingira ya kimataifa yamebadilika na kwamba uhusiano kati ya Iran na Urusi umeendelea kuimarika.

Mamlaka ya Iran imeeleza kuwa ushirikiano wa kijeshi kati yake na Urusi unazidi kuwa mzuri kila siku. Iran ilisema mwezi Novemba kwamba ilikamilisha mipango na Urusi ya kuipa ndege za kivita aina ya Su-35 na helikopta aina ya Mi-28.