Urusi na Marekani kuandaa mkutano kuhusu Syria
8 Mei 2013Marekani na Urusi zilikubaliana kuandaa mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani nchini Syria. Katika mazungumzo yaliyoingia hadi saa za usiku, Waziri wa Mamo ya Nchi za nje wa Marekani John Kerry alikutana kwanza kwa zaidi ya saa mbili na Rais wa Urusi Vladmir Putin na kisha akafanya mazungumzo yaliyodumu saa tatu na Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov.
Lavrov na Kerry wamesema wanataraji kuandaa kongamano la kimataifa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu ili kuufuatilia muafaka wa Geneva uliotiwa saini na nchi zenye nguvu duniani mwezi Juni mwaka jana wa kuwepo suluhisho la amani nchini Syria.
Kuufufua muafaka wa Geneva
Makubaliano ya Geneva, ambayo hayakutekelezwa, yaliweka njia ya kuundwa serikali ya mpito bila ya kufafanua hatima ya Rais Bashar al Assad. Kerry amesema mpango huo wa vifungu sita uliosimamiwa kwa mara ya mwisho na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Koffi Annan, unapaswa kuwa mkakati ambao watu wa Syria wanapaswa kutumia katika kulipata taifa jipya na ambao utamaliza umwagaji damu, na mauwaji ya kikatili.
Lavrov amesema Urusi na Marekani ziko tayari kutumia raslimali zao zote kuzileta pamoja pande za serikali na upinzani katika meza ya mazungumzo. Urusi kwa muda mrefu imekuwa ikizishutumu nchi za magharibi kwa kuuchochea hata zaidi mgogoro wa Syria. Nayo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinaishutumu Urusi kwa kushindwa kutumia ushawishi wake kwa utawala wa Syria kusitisha umwagaji damu na kumpa silaha rais Assad. Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Lakhdar Brahmi ameutaja mpango huo wa Urusi na Marekani kuwa ni “hatua ya kwanza kubwa”.
Wakati huo huo waasi wa Syria wamesema wamewakamata wanajeshi wanne wa kulinda amani raia wa Ufilipino katika milima ya Golan, ikiwa ni mara ya pili katika miezi miwili kwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kutekwa katika eneo hilo la kusimamisha mapigano baina ya Syria na Israel.
Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Iran Ali Akbar Salehi alifanya ziara ya ghafla mjini Damascus jana jioni kwa mazungumzo na Rais Bashar al Assad. Baadaye alisema nchi yake itasimama na Syria ili kukabiliana na mashambulizi ya Israel. Iran ni mshirika wa karibu wa Assad, na inashutumiwa na upinzani kwa kuyatuma majeshi na washauri kuunga mkono utawala.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Ssessanga, Iddi Ismail