Urusi na Ukraine zadai kupata mafanikio makubwa vitani
10 Machi 2026
Maafisa wa Urusi na Ukraine wanatoa madai yanayokinzana ya mafanikio katika vita vyao ambavyo vimedumu sasa kwa miaka minne huku Ukraine ikisema imevirudisha nyuma vikosi vya Urusi katika baadhi ya maeneo kwenye mstari wa mbele wa vita na ikulu ya Kremlin nayo ikisisitiza kuwa uvamizi wake nchini Ukraine unapiga hatua.
Kiev imesema imefanikiwa kudungua droni 122 kati 137 zilizovurumishwa na Urusi na kusema kuwa watu 14 wakiwemo watoto wamejeruhiwa.
Ukraine yasema imekomboa eneo la karibu kilomita za mraba 400
Wakati huo huo, mkuu wa chombo kinachosimamia utendaji wa vikosi vya jeshi nchini Ukraine Jenerali Oleksandr Komarenko ameliambia shirika la habari la RBC-Ukraine kwamba vikosi vyake vimekomboa eneo la karibu kilomita za mraba 400 kutoka kwa uvamizi wa Urusi katika wiki za hivi karibuni na sasa vinadhibiti karibu Dnipropetrovsk yote.
Katika taarifa aliyotoa leo, Komarenko amesema ni makazi matatu tu madogo katika eneo la kusini mwa Ukraine ambayo yamesalia chini ya udhibiti wa Urusi, na mengine mawili yakisubiri kukaguliwa.
Ameongeza kuwa mwezi Februari ulishuhudia matokeo chanya na kwamba maeneo mengi zaidi yalikombolewa ikilinganishwa na yaliotekwa. Komarenko amekiri kwamba hali jumla ni tete lakini iko chini ya udhibiti.
Huku hayo yakijiri, mshauri wa mambo ya nje wa ikulu ya Urusi Yuri Ushakov amewaambia waandishi wa habari kwamba rais wa nchi hiyo Vladimir Putin amemwambia mwenzake wa Marekani Donald Trump kwamba vikosi vya Urusi vinapiga hatua muhimu nchini Ukraine.
"Hali ya sasa kwenye mstari wa mbele wa vita ilielezewa, ambapo vikosi vya Urusi vinasonga mbele kwa mafanikio makubwa. Kama ilivyobainishwa, hii ni sababu ambayo inapaswa kuhimiza serikali ya Kyiv hatimaye kutumia njia ya mazungumzo kusuluhisha mzozo ulioko."
Mamlaka ya Urusi yadaiwa kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu
Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Ukraine, imesema ushahidi uliokusanywa unaiwezesha kuhitimisha kwamba mamlaka ya Urusi ilifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuwafukuza na kuwahamisha kwa nguvu, pamoja na kuwapoteza watoto.
Uchunguzi huo umeonyesha kuwa Urusi iliwahamisha ama kuwafukuza maelfu ya watoto kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukraine.
Hadi sasa, tume hiyo imethibitisha kufukuzwa au kuhamishwa kwa watoto 1,205 na kwamba miaka minne baadaye, asilimia 80 ya watoto waliofukuzwa au kuhamishwa katika visa vilivyochunguzwa na tume hiyo hawajarejea.
Urusi haiitambui tume hiyo na haijajibu maombi ya kutoa maelezo.